KYELA: Kisa kifuatacho ni uthibitisho tosha kwamba, mke wa mtu ni sumu, Gazeti la IJUMAA lina kisa na mkasa. ‘NJOO MUME WANGU HAYUPO’ Mkazi wa Kitongoji cha Bondeni ‘B’ Ubalozi Namba 5 Wilaya Kyela jijini Mbeya, Onesmo Nombo (35), yamemfika mazito kisa kuambiwa; “Njoo nyumbani mume wangu hayupo!”
Onesmo amejikuta akinusa kifo laivu, baada ya kufanyiwa kitu mbaya kwa kushushiwa kipigo cha mbwa koko chumbani kwa jirani yake, baada ya kufumaniwa akimnyemelea mke wa mtu, ambaye anadaiwa kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi.
SAA 7:00 USIKU
Katika tukio hilo lililojiri saa 7:00 usiku hivi karibuni na kusababisha taharuki kwenye kitongoji hicho cha Bondeni ‘B’ Ubalozi Namba 5 Wilaya Kyela jijini Mbeya, inaelezwa na mashuhuda kwamba, mwenye mke, Owden Erasto alimuaga mkewe usiku huo kuwa, anakwenda kuchimba dawa ya tumbo.
Kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Gazeti la IJUMAA lilipotinga kwenye kitongoji hicho, tukio hilo limeacha gumzo katika nyumba ya Erasto aliyedai kumfumania Nombo na mkewe kisha kumpa kipigo ‘hevi’.
KUMBE NI MTEGO
Imeelezwa kuwa, shukrani ziende kwa wasamaria wema waliomuokoa Nombo akiwa hoi kwa kipigo, akituhumiwa kumnyemelea mke wa Erasto bila kujua kuwa aliwekewa mtego.
MJUMBE AFUNGUKA
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA, Mjumbe wa Nyumba Kumi, Herufi Mwakibinga, alifunguka kuwa, alifuatwa na mke wa Nombo aitwaye Happy Nombo, akieleza kuwa nyumbani kwao kuna ugomvi mkubwa.
Alisema kuwa, alipofika alipiga mayowe baada ya kukuta watu hao wanataka kuuana, ndipo majirani walipofika kwa wingi na kufanikiwa kuutatua ugomvi huo.
Alisema, baada ya hapo alishangaa kuona katika chumba cha Erasto kuna kisu, nondo na nyembe vilivyoandaliwa kumshambulia mgoni huyo, kwani alitengeneza mtego, baada ya kukuta meseji kwenye simu ya mke wake wakati mkewe amelala, meseji iliyosomeka; “Ameondoka nije?”
Inaelezwa kwamba, Erasto (mwenye mke) aliijibu SMS hiyo; “Njoo mume wangu hayupo…”
Baada ya kujibiwa hivyo, mgoni huyo alifika katika nyumba hiyo na kuandika tena meseji; “Zima taa…” huku akidhani anachati na mke wa mtu ambaye ni hawara yake, kumbe anachati na mwanaume mwenzake bila kujua.
VITA NZITO, WANG’OANA MENO
Alisema kuwa baada ya taa kuzimwa, aliingia moja kwa moja chumbani, ndipo alipokiona cha mtema kuni kwa kushushiwa kichapo, huku naye akijihami kwa kujibu mashambulizi, hali iliyosababisha kuumizana na hata kung’oana meno.
Mwakibinga aliongeza kuwa, baada ya watu kujaa katika nyumba hiyo, mke wa aliyefumaniwa alifika na kushangaa kumuona mumewe akiwa chini ya ulinzi, tena chumbani kwa watu, huku akimuuliza hapo ndipo alipokwenda kuchimba dawa? Swali lililokosa jibu.
Baada ya hapo, Mwakibinga alisema, aliamua kumpa taarifa mwenyekiti wa kitongoji hicho, David Mwakakongobe ambaye naye alifika eneo la tukio na baadaye watu hao ambao ni majirani, walipelekwa Polisi na kupewa hati ya kupatiwa matibabu (PF-3) na kesho yake walikwenda kuripoti Polisi.
NI FEDHEHA
Mwakakongobe, licha ya kulaani kitendo hicho, pia aliwataka wananchi waishi kwa upendo bila kuwa na tabia ya kuibiana wake za watu, kwani kitendo cha Nombo kutembea na mke wa mtu, ni cha fedheha.
Aliongeza kuwa, suala la wawili hao linakwenda mahakamani kwa kuwa Jeshi la Polisi liliwapa mwongozo kuwa kesi hiyo, ni ya madai, hivyo wameamua kuiachia mahakama ili ishughulike na jambo hilo.
Happy Nombo kwa upande wake, alimtuhumu mumewe kwa kitendo hicho na kusema kuwa, ni cha aibu kwani siku ya tukio, saa saba usiku alijifanya anaumwa tumbo na kumuaga kuwa anakwenda kuchimba dawa kwenye uwanja wa Takoshiri na baada ya dakika kumi, alishangaa kuona amefumaniwa chumbani kwa watu.
Alisema ni jambo la aibu kubwa mtaani kwao, kwani hakutegemea kama mumewe anaweza kutembea na mke wa mtu, tena jirani na kwamba kwa sasa hatamuamini mumewe kwa kuwa alionesha tamaa kubwa kwa kumuacha kitandani usiku wa manane na kwenda kunyemelea wake za watu.
Erasto alisema kuwa, alipata taarifa kuhusu Nombo kutembea na mke wake, ndipo alipoweka mtego kwa kupekua simu ya mkewe na kufanikisha kumkamata na kwamba, alikuwa akiibiwa kutokana na yeye kushinda kijijini kulima.
Alisema kuwa, baada ya fumanizi hilo, mkewe Martha Kyuja alikimbia akiwa na kipande cha kanga usiku huohuo na hadi leo hajulikani alipo na kwamba, kuna uwezekano akakimbilia kijijini kwao, Stamico huku akieleza kuwa hana sababu ya kumtafuta, kwani tayari amejifukuza.
Mke wa kiongozi mmoja mstaafu kijijini humo, ambaye aliomba jina lake lisichorwe gazetini, alisema kijana huyo amewadhalilisha wanaume na pia mwanamke huyo amewadhalilisha wanawake, kwani haiwezekani mwanaume atembee na mke wa mtu, tena chumbani kwake wakati mtaa huo una wajane wengi.
KAMA BABA MWENYE NYUMBA
Alisema kuwa, ilifikia mahali kijana huyo alikuwa anafika nyumbani kwa mwenziye huku akila ugali na kulala katika kitanda cha mwenziye kama baba mwenye nyumba, huku akiwadanganya watoto kwa kuwapa juisi na wakimuita mjomba, jambo ambalo liliwahuzunisha na ndipo walipotoa taarifa kwa mwenye mke ambaye aliweka mtego na kufanikiwa kumnasa.
Gazeti la IJUMAA lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, ACP Ulrich Matei, ambaye aliahidi kulifuatilia sakata hilo.
STORI: IBRAHIM YASSIN, IJUMAA
