×

JPM: Tunataka Malawi Waamue Wenyewe – Video

Rais  John  Magufuli akipiga makofi wakati akisikiliza hotuba ya mgeni wake Rais  Malawi  Lazarus McCarthy Chakwera,  wakati walipokuwa wazungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam leo tarehe 07 Oktoba 2020.

RAIS wa  Malawi, Lazarus McCarthy Chakwera, ameendelea na ziara yake ya siku tatu nchini kuanzia jana  Oktoba 07,  2020,  yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi ya Tanzania na Malawi katika masuala ya kibiashara ambapo alipokelewa na mwenyeji wake Rais John Magufuli.

 

Baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Magufuli ameeleza namna walivyokubaliana kushirikiana kukuza uchumi wa wananchi wa Tanzania na Malawi katika sekta ya biashara na miundombinu.

Alisema kuwa katika mazungumzo yao ya muda mfupi wamekubaliana kuanzishwa kwa ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) mjini Lilongwe ambayo itasogeza huduma za wafanyabiashara kutoka Malawi.

“Tumezungumza na Mheshimiwa Rais wa Malawi kwamba upande wa Malawi waziri anayehusika na usafirishaji ahakikishe kuwa anawezesha mambo yaliyokuwa yamekwama hususani ufunguzi wa ofisi za TPA mjini Lilongwe,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli alitoa wito kwa Rais Chakwera kuwa mahusiano kati ya nchi hizo mbili yanatakiwa yawe ni mahusiano ya kibiashara ambayo kwa kiasi kikubwa yatawezesha kukua kwa uchumi kati ya Tanzania na Malawi.

Katika Sekta ya usafirishaji,  Magufuli alieleza mambo yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwemo kuimarishwa kwa sekta ya usafiri wa anga, kwani sekta hiyo ni kiungo muhimu katika mahusiano ya kimataifa hasa kwa Tanzania na Malawi kama wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

“Tunataka Malawi waamue wenyewe wanataka kutumia usafiri wa njia gani, kwa njia ya treni, barabara, ndege au bandari na ndiyo maana tunataka ule mkataba uliokuwa haujakamilika kati ya Malawi na Tanzania kuhusu usafiri wa ndege umalizwe haraka kwa sababu sekta hii ni muhimu kwa utalii,” amesema Magufuli.

 

Aliongeza kuwa sekta ya umeme ni muhimu kwa nchi hizo mbili kwa hiyo wataangalia jinsi gani wataweza kushirikiana katika ujenzi wa mradi wa umeme wa Songwe ambao utatarajiwa kuzalisha megawatt 180, kwani Tanzania ina uzoefu mkubwa wa ujenzi wa miradi kama hiyo ikiwa inatekeleza ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere Hyroelectric Power (JNHPP), wenye kuzalisha Mg 2,115.

 

Kwa upande wake, Chakwera amesema kuwa ni muda sasa kwa Waafrika kuungana na kufanya maendeleo ya pamoja kama ndugu ili kukuza uchumi wa nchi za Afrika na bara kwa ujumla.

 

 

 

 

Rais wa Jamhuri ya Malawi Mheshimiwa Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera wakati akizungumza na wanahabari kutoka Tanzania na Malawi.

PICHA NA IKULU.

“Ni muda sasa kwa Waafrika kutafuta mwelekeo wetu na kufanya maendeleo kwa kasi yetu, kuliko kusubiri watu wengine waje kufanya haya, hii itasbabisha kuwepo na uhusiano mzuri na mwenendo mzuri wa kibiashara ambao utaleta uwazi katika biashara na kupelekea matumizi ya pamoja ya rasilimali zetu,” amsema Chakwera.

 

Aidha  alimshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha na kubadilishana mawazo kuhusu ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo siasa, uchumi na sekta za uzalishaji madini ili kuinua uchumi wa wananchi wa Tanzania na Malawi.

Na.Beatrice Sanga-MAELEZO

Leave a Comment