IMEELEZWA kuwa, Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze raia wa Burundi, tayari ameanza kazi ya kukinoa kikosi hicho kwa kutuma programu zake kwa kocha msaidizi, Juma Mwambusi.
Kaze ambaye ameshafi kia makubaliano na Yanga kuinoa timu hiyo akichukua mikoba ya Zlatko Krmpotic raia wa Serbia aliyetimuliwa hivi karibuni, anasubiriwa kutua tu ambapo taarifa kutoka Yanga zinasema kwamba, Alhamisi ijayo ya Oktoba 15, mwaka huu atakuwa katika ardhi ya Tanzania akitokea Canada.
Chanzo kutoka katika benchi la ufundi la Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa: “Mara kwa mara Kaze anawasiliana na Mwambusi ili kufahamu kikosi kinaendeleaje, amekuwa akituma program anazotaka wachezaji wapatiwe na Mwambusi anazifanyia kazi.
“Hata mechi ya kirafi ki ambayo Yanga imecheza dhidi ya Mwadui yeye ndiye amependekeza, pia amekuwa akiwafuatilia wachezaji katika mechi za nyuma kupitia video za mechi zao.”
GSM YAMFUNGUKIA
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, Injinia Hersi Said, amezungumzia ujio wa Kaze akisema: “Kocha ataondoka Canada Jumatano ya wiki ijayo na kuwasili Tanzania Alhamisi tayari kwa ajili ya kukinoa kikosi chetu.”
STRAIKA SIMBA AITAMANI YANGA YA KAZE
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo, amefunguka kuwa, Yanga ina bahati kubwa ya kumnasa kocha huyo ambaye ana uwezo mkubwa wa kuiandaa timu na ikacheza soka safi uwanja wowote ule.
“Shida ya nchi zetu hizi za Afrika zina viwanja vingi ambavyo vimekosa ubora wa kutosha, lakini bado naamini Yanga wataona faida ya kuwa na Kaze kwa sababu timu itaweza kucheza soka la kuvutia kwa pasi nyingi katika uwanja wowote ambao watakwenda kucheza.
“Uzuri nimecheza hapo Tanzania na naelewa lakini nimefanya kazi na kocha Kaze wakati nilipokuwa Atletico, naongea kitu ambacho nakijua juu yake, yeye mwenyewe pia siyo mgeni na mazingira ya Tanzania pamoja na mpira wake, hivyo mashabiki wa Yanga watarajie makubwa kutoka kwake. Naiona Yanga ikifanya vizuri chini yake,” alisema Mavugo

