MWENYEKITI wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF), Wakili Kichere Mwita Waissaka amesema kuwa suala la mchezaji wa Simba, Bernard Morrison lililowasilishwa kwenye kamati hiyo halijasikilizwa kwa kuwa mchezaji huyo alituma wawakilishi.
Waissaka amesema kuwa yapo mambo ambayo yanapaswa kuwakilishwa na wawakilishi lakini kwenye suala la Morrison ambalo ni la kimaadili alipaswa awepo yeye mwenyewe ili aweze kuyajibu maswali mengine ambayo hayawezwi kujibiwa na wawakilishi.
Waissaka amesema:- “Mashtaka dhidi ya Bernard Morrison kifupi ni kwamba mlalamikiwa hakufika mwenyewe alitoa udhuru ni sababu iliyofanya kamati ikashindwa kuskiliza hukumu kwa kuwa alisema yupo na Klabu ya Simba.
“Hata hivyo alituma wawakilishi wawili ambao ni wanasheria hata hivyo kamati iliona kwamba ni haki mlalamikiwa mwenyewe awepo hivyo kamati iliamua kuahirisha suala hilo.
“Sababu kuna maswali mengine yalipaswa yajibiwe na mchezaji mwenyewe na sio wawakilishi hivyo wangeshindwa kujibu.
“Pia kamati iliarifiwa kwamba suala la Morrison limeripotiwa kwenye mahakama ya usuluhishi ya Fifa lakini ieleweke pia iliyokatiwa rufaa ni kwenye masuala ya usajili kwenye masuala ya maamuzi ya usajili ambao wamekatiwa rufaa ni kamati ya usajili kwenye Cas, chombo hiki kipo Uswisi.
“Suala lililoletwa mbele ya kamati yetu ni la maadili isipokuwa masuala ya usajili yameripotiwa huko mbele kwenye kamati ya Cas.” amesema.
Morrison yupo kwenye mvutano na Klabu yake ya Yanga kwenye suala la mkataba wake ambapo Yanga waajiri wake wa zamani wanaeleza kuwa alikuwa na mkataba wa miaka miwili huku yeye akidai kuwa alikuwa na kandarasi ya miezi sita.
Sakata hilo lilisikilizwa TFF na aliweza kushinda kwa kile kilichoelezwa kuwa mkataba ulikuwa na mapungufu kati yake na waajiri wake jambo lililomfanya awe huru kuchagua timu anayokwenda kuitumikia.
Kutokana na majibu hayo Yanga walieleza kuwa wanakwenda Cas kukata rufaa ili kupata haki juu ya mchezaji huyo.
