RAIS John Magufuli amesema kuwa ataitangaza siku ya uchaguzi mkuu, Oktoba 28, 2020 kuwa siku ya mapumziko ili wananchi wote wenye sifa wakapige kura kuchagua viongozi wanaowataka kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Magufuli ambaye pia ni mgombea urais kupitia chama hicho amesema hayo leo Jumatano, Oktoba 14, katika Viwanja vya Tanganyika Packers wakati akifanya mkutano wake wa kampeni kwa majimbo ya Wilaya ya Kinondoni ambayo ni Kawe na Kinondoni.
“Namaliza kampeni zangu Dar nikiwa na furaha sana, nimependa kupita maeneo mengine kama Mbagala na Ukonga, lakini nitamtuma Mzee Kikwete huko Katavi; Rukwa nimemtuma Mama Samia, Mtwara na Lindi nitamtuma Kassim Majaliwa, ningependa nifike Morogoro, Pwani na Pemba.
“Uchaguzi wa mwaka hautaingilia siku za ibada, utakuwa Jumatano, Oktoba 28, na siku hiyo nitaitangaza iwe siku ya mapumziko, lakini ukapige kura kwanza halafu urudi ukapumzike.
“Huu ni mwaka wa kuamua na kutengeneza Tanzania mpya, Oktoba 28 tukafanye ya kweli kwa ajili ya Taifa hili, msidanganywe kwamba Magufuli ameshashinda, siwezi kushinda bila kupigiwa kura, hata kama anaumwa, mpeleke akapige kura.
“Mkutano mkubwa kama huu utalinganisha na vimikutano vyao? Wanasema watu wanajaa sababu ya wasanii, akina Mwamposa na Mashehe wamekuja kucheza ‘ndombolo’? Wasanii wanaipenda CCM, kuna kosa wakiwa wananchama wa CCM? Wamekuja kujumuika na wananchama wenzao kusherehekea,” amesema Magufuli.

