BAADA ya kukamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Burundi, Saidi Ntibazonkiza, kocha mkuu mpya wa Yanga, Cedric Kaze anayetarajia kutua hapa nchini leo Alhamisi, amependekeza usajili wa kiungo, Cedric Amissi.
Amissi alikuwepo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Burundi kilichocheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars, wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam uliomalizika kwa Stars kufungwa bao 1-0.
Yanga inataka kumsajili kiungo huyo raia wa Burundi mwenye uwezo wa kuuchezea mpira kwa ajili ya kuiimarisha safu yao ya kiungo katika kuhakikisha wanarudisha utawala wao kwenye Ligi Kuu Bara.

Kaze ambaye anatokea Canada ambapo alikuwa akiishi huko, anatarajiwa kuwasili leo Alhamisi majira ya saa 4 usiku kwa ndege ya Shirika la KLM.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Kaze raia wa Burundi, ametoa mapendekezo ya kumsajili kiungo huyo anayeichezea Al-Taawoun inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, kocha huyo ndiye aliyependekeza usajili wa Ntibazonkiza aliyeisumbua safu ya ulinzi ya Stars iliyoongozwa na Bakari Mwamnyeto na Abdallah Kheri kabla ya kufunga bao la ushindi katika mchezo huo wa kirafiki.
Aliongeza kuwa, kiungo huyo atasaini mkataba wa kuichezea Yanga kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika hivi karibuni ambaye huenda akajiunga katika dirisha dogo la usajili.
“Kocha akiwa bado yupo Canada alipendekeza usajili wa Ntibazonkiza ambaye hivi sasa ni mchezaji huru anayeruhusiwa kuichezea Yanga muda wowote.“Kaze pia amependekeza usajili wa kiungo Cedric ambaye alikuwepo kwenye kikosi cha Burundi akiwa amevaa jezi namba 17.
“Hivyo, kiungo huyo ambaye ni kipenzi cha Kaze wakati wowote GSM watamsajili katika kukiimarisha kikosi ili kufikia malengo yake,” alisema mtoa taarifa huyo.Alipotafutwa Mkurugenzi Uwekezaji wa GSM ambaye pia Mjumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hersi Said kuzungumzia hilo, alisema: “Hizo taarifa kwangu ni mpya, hivyo tusubirie muda ukifika kama lipo tutaliweka wazi.”
STORI: WILBERT MOLANDI, Dar

