×

JPM Atua Bagamoyo, Asema Watakaoshindwa Wameshajijua – Video

MGOMBEA urais Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Mhe. Dkt.John Pombe Magufuli  amezungumza na Wananchi wa Bagamoyo katika uwanja wa Mwanakalenge wakati akiwa njiani kuelekea Mkoani Tanga leo Jumatatu Oktoba 19, 2020.

 

Akizungumza katika mkutano huo uliohdhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja viongozi mbalimbali akiwemo Rais Mstaafu na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Dkt. Jakaya Kikwete.

 

“Mwaka 2015 nilifika hapa Bagamoyo kuomba kura. Leo tena tumekuja kuwaomba tena kura kwa sababu katika miaka 5 iliyopita tumeshirikiana pamoja kupata mafanikio haya makubwa ambayo tumeyaona. Nimekuja leo wana Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kuwaomba kura kwa sababu kuu mbili, moja ni kwa namna tulivyoshirikiana kuleta maendeleo

 

“Kwa miaka kumi yote, Mzee Kikwete aliteua mimi kuwa Waziri wake, nimejifunza mengi kutoka kwake. Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais tulikuwa 42, Mzee Kikwete aliendesha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa hadi nikapatikana mimi. Ahsante sana kwa upendo mkubwa.

 

“Vijana msidanganywe na vitu vya bure vya kuambiwa mjipange barabarani, zipo nchi ambazo mpaka leo zipo kwenye vita, usijiangalie wewe tu muangalie mdogo wako, mama yako uliyemuacha nyumbani kama ataweza kukimbia kama wewe.

 

“Hakuna kitu kizuri duniani kama amani, tukikosa amani hakuna chochote tutakachofanya hata ukiwa na mpenzi wako utamkimbia, una msikiti au kanisa lako utalikimbia, nitasikitika sana kuona Watanzania wanaumizana sababu ya uchaguzi.

 

“Uchaguzi wa mwaka huu utaamua tuwe na viongozi watakaolinda uhuru wetu au kuwa na viongozi ambao ni vibaraka au makuwadi wa mabeberu, pia uchaguzi utaamua tuwe na viongozi wenye dhamira ya kweli ya kutetea wanyonge au kuwa na viongozi ambao ni matapeli wa siasa.

 

“Tuchague salama na ninajua wa kushindwa wameshajijua kama watashindwa msikubali kamwe, akikuambia kuandamana mwambie aende yeye na mke wake na baba yake, wakaandamane, yako maisha hata baada ya uchaguzi. Ukiona mtu anahubiri uvunjifu wa amani, ujue kwamba ameshashindwa. Hata vitabu vitakatifu vinahubiri juu ya amani, amani ni kitu cha muhimu sana.

 

“Huwezi kuelewa hawa watu waliokaa nje wameweka mikataba gani, mtu anasimama anasema barabara hii haina maana, kweli haina maana? Na nyinyi wananchi mnakaa mnashangilia kweli?

 

“Tunahitaji kujenga taifa letu, taifa lenye amani. Na kwa kweli Mungu anatupenda sana, palitokea Corona tulimuomba Mungu na akatusikia, wenzetu walisema tutaokota maiti barabarani, na wengine wakakimbia hata bungeni, lakini Mungu akatusikia.

 

“Nawapongeza sana viongozi wa Mkoa wa Pwani kwa kufanikisha ujenzi wa viwanda vingi, Mkoa wa Pwani ndiyo unaongoza kuwa na viwanda vingi nchini, mwaka 2015 mkoa wa Pwani ulikuwa na viwanda 395 lakini sasa una viwanda 1,236 na kutoa ajira zaidi ya 200,000.

 

“Kutokana na kupanuka kwa wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla jinsi unavyong’ara hususan kwa ujenzi wa viwanda, nimeamua kuwa nitakapochaguliwa nitaifanya Chalinze kuwa wilaya ili maendeleo yafanyike kwa kasi kubwa,” amesema Magufuli.

 

Leave a Comment