AKIENDELEZA rekodi ya kutupia mabao, straika wa Simba, Mkongomani Chris Mugalu, ametamba kwamba anaweza kuivunja rekodi ya straika wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ ya kufunga mabao mengi kwa msimu mmoja.
Mugalu ameongeza anaweza kuvunja rekodi hiyo ya Mmachinga ya kufunga mabao 26 ndani ya msimu endapo tu kocha wake Sven Vandenbroeck ataendelea kumpa nafasi kikosi cha kwanza.
Mmachinga ndiye anashikilia rekodi ya mchezaji wa Ligi Kuu Bara kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja ambapo alifanya hivyo mwaka 1999 akipachika mabao 26.
Kwa sasa, Mugalu aliyetua Simba akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, amefunga mabao matatu kwenye ligi huku akiwa na mabao saba ya jumla ikiwemo na mechi za kirafiki.
Mabao hayo aliyafunga dhidi ya Mlandege kwenye mechi ya kirafiki akifunga mawili, Vital’O katika Simba Day (moja), African Lyon (moja) na ligi mbele ya Biashara United, Gwambina na JKT Tanzania.
Staa huyo ameliambia Championi Jumatatu, kuwa kwake kama akiendelea kuaminiwa kwenye kikosi cha kwanza, ana nafasi kubwa ya kufunga na kuifikia rekodi hiyo ya Mmachinga.
“Kuhusu kufunga idadi hiyo ya mabao na kuivunja, inawezekana kabisa endapo tu kocha ataendelea kunipatia nafasi ya kucheza mara kwa mara.
“Nikiwa na uhakika wa kucheza basi siyo jambo gumu sana kufikia idadi hiyo ya mabao, kwa sababu naamini ninaweza kufunga katika kila nafasi ambayo nitapata,” alisema Mkongomani huyo.
SAID ALLY NA JOEL THOMAS,Dar es Salaam
