KOCHA wa Yanga, Mrundi, Cedric Kaze, amefunguka kuwa anafurahishwa na mshambuliaji wa kati wa timu hiyo, Wazir Junior kutokana na kuwa na faida nyingi anapokuwa uwanjani katika nafasi anayocheza.
Kaze ametoa kauli hiyo kufuatia mshambuliaji huyo kufunga bao la ushindi katika mchezo dhidi KMC uliopigwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Akizungumza na Championi Jumatano,Kaze alisema kuwa mshambuliaji huyo ni mmoja kati ya wachezaji wanaomfurahisha kutokana na kufanya kazi zaidi ya moja katika nafasi anayocheza.
“Wazir ni mchezaji mzuri kwa sababu akiwa uwanjani anakupa vitu vingi, timu inapokuwa inashambuliwa anarudi chini kuja kusaidia kukaba licha ya kuwa mshambuliaji wa kati na wakati huohuo bado anatimiza majukumu yake kwangu, huyu ni bora hadi sasa.
“Naona ni mchezaji mzuri mwenye uwezo wa juu sana na bado ana umri wa kwenda mbali zaidi, amekuwa na juhudi za kujituma kuanzia kwenye mazoezi, ananifurahisha na ni wakati wa kufanya kile ambacho anakiona kwa ajili ya timu,” alisema Kaze.
Katika kikosi cha Yanga, mshambuliaji huyo ndiye pekee mzawa ambaye amefanikiwa kufunga bao hadi sasa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na anaonekana kuwa anaweza kufanya vizuri zaidi huko mbele.


