ABDALLAH Mwinyimkuu wa Singida ndiye mwamuzi anayetarajiwa kuchezesha mchezo wa leo Jumamosi kati ya Yanga na Simba lakini rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ndiyo wamekuwa na bahati kubwa ya kupata matokeo ya ushindi katika mechi zilizochezeshwa na mwamuzi hiyo.
Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imepitisha jina la mwamuzi huyo kuchezesha mchezo huo katika waamuzi sita walioteuliwa kusimamia mchezo huo wenye upinzani mkali. Yanga na Simba ambao wanatarajia kucheza leo Jumamosi utakuwa mchezo wa kwanza kwa msimu huu kukutana kwenye Ligi Kuu Bara.
Tayari TFF imeachia majina ya waamuzi sita watakaochezesheza mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini ambao ni Elly Sasii, Mohamed Mkono, Frank Komba, Abdallah Mwinyimkuu, Abubakar Mturo na Ramadhani Kayoko wakati Kamishna wa mchezo akiwa Philip Alando na mtathmini wa waamuzi akiwa ni Pascal Chiganga.
Uchunguzi uliofanywa na Championi umebaini kuwa Mwinyimkuu ndiye atachezesha mchezo huo baada ya jina lake kupitishwa na viongozi wa juu wa Bodi ya Ligi na TFF kwa ajili ya mchezo huo huku msimu huu akiwa amechezesha mechi mbili za Simba na Yanga katika Ligi Kuu Bara.
Mwinyimkuu alichezesha mechi yake kwanza kwa timu hizo kati ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo ambao Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Tonombe Mkukoko. Kwa upande wa Simba, mwamuzi huyu kutoka Singida alichezesha mchezo mmoja ambao vijana hao wa Msimbazi walilala kwa bao 1-0 mbele ya Ruvu Shooting bao ambalo liliwekwa kimiani na Fullu Zullu Maganga.
Hii itakuwa ni mechi yake kwanza kubwa ambayo inazikutunanisha Yanga na Simba baada ya jina lake kupenya katika mchakato mkali wa majina yaliotangazwa na TFF.
Ibrahim Mussa, Dar es salaam
