×

Sven Alia na Penalti

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, amesema kuwa timu yao ilistahili kupata penalti katika mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar, juzi.

 

Katika mchezo huo wa dabi ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, Yanga ndio walikuwa wenyeji wa mchezo huo ambapo mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, kocha Sven alisema kuwa wapinzani wao Yanga walicheza madhambi mengi ndani ya eneo lao la hatari hivyo walitakiwa kupata penalti lakini refa hakuwa upande wao.

 

“Nafi kiri tulistahili kupata penalti katika mchezo huu, kwa kuwa kuna madhambi mengi wapinzani wetu waliyacheza wakiwa katika eneo lao la hatari ila nitaenda kujihakikishia vizuri kwa kuangalia marudio ya mechi hii.

 

“Bado naamini kuwa tulicheza vizuri na tulistahili kuibuka washindi wa mechi hii ila mwisho wa siku tutaishia kusema kuwa tulikuwa na siku mbaya kazini,” alisema kocha huyo.

 

Baada ya sare hiyo, Simba inabaki kwenye nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 20 huku Azam FC wakiwa ndio vinara wa ligi wakiwa na pointi 25 wakifuatiwa na Yanga wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 24 katika michezo kumi waliyocheza timu zote.

Marco Mzumbe, Dar es Salaam

Leave a Comment