MUUZA sura (video queen) kwenye video za wasanii wa Bongo Fleva, Nabila Aslam ‘Nanah’ aliyeonekana kwenye video ya Wimbo wa I Love You wa msanii Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ ameibuka na mambo mazito.
Kama utakumbuka, kipindi kile wakati video hiyo inatoka miezi kadhaa iliyopita, kuliibuka maneno mengi kuwa huwenda wawili hao walishiriki tendo la ndoa. Lakini kumbe skendo ile ilimsababishia Nanah msala mzito kiasi cha kuvunjika kwa uchumba wake.
Kufuatia ishu hiyo, Nanah alijikuta hakubaliki tena ukweni hadi leo. Mtu wa karibu wa Nanah ambaye hakuwa tayari jina lichorwe gazetini ameeleza kuwa, tangu kipindi kile uhusiano wake na wakwe zake haujawahi kuwa mzuri tena, hali iliyosababisha kuvunjika kwa uchumba na mzazi mwenzake.
“Unajua ile video ya Rayvanny ilimsababishia Nanah matatizo makubwa sana pamoja na kwamba ndiyo iliyomtambulisha kwa watu, lakini kwa upande wa familia, mambo hayakuwa mazuri.
“Unaambiwa siku hizi Nanah amekuwa kama Hamisa Mobetto na Mama Dangote, yaani wakwe zake hawataki hata kumuona.
“Wanadai kuwa amewaaibisha kwa kutembea na Rayvanny na kumsaliti mtoto wao na kilichowafanya waamini kuwa ni kweli mkwe wao alimsaliti kijana wao, ni pale ambapo waliona kondomu kwenye kitanda wakati video hiyo inashutiwa.
“Hivi ninavyokuambia, Nanah ameshaachana na mchumba’ke kwa sababu hiyo,” anasema mtoa habari huyo.
Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa mengi, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta Nanah na kufanya naye mahojiano maalum ambapo amezungumza mambo mengi ikiwemo ishu hiyo na kutaka kujua ukweli wa hayo yanayosemwa, Kwa upande wake, Nanah anakiri kutengana na baba wa mtoto wake na kusema kuwa, hakuwa na ukaribu na wakwe zake hao hivyo hata wasipompenda hana shida.
IJUMAA WIKIENDA: Mambo Nanah…
NANAH: Poa tu karibu…
IJUMAA WIKIENDA: Hivi bado upo kwenye ndoa?
NANAH: Hapana, sijaolewa na wala sijawahi kuwa kwenye ndoa.
IJUMAA WIKIENDA: Mbona tuliona hadi picha kabisa za ndoa, tena uliposti wewe mwenyewe?
NANAH: Kweli tena nakuambia, mimi sijaolewa ila tu nilikuwa kwenye uhusiano ambao ulikuwa siriazi (uchumba).
IJUMAA WIKIENDA: Unaposema ulikuwa kwenye uhusiano, hapo unamaanisha nini? Kwani Mmeshaachana? Nanah: Ndiyo, tumeshaachana na sasa hivi nipo kwenye uhusiano mpya.
IJUMAA WIKIENDA: Ina maana umeachana na baba wa mtoto wako?
NANAH: Ndiyo…
IJUMAA WIKIENDA: Ni kweli kwamba umeachana na baba wa mtoto wako kwa sababu ya ile video na Rayvanny? Kwa sababu kuna maneno yanayosemwa kwamba hupatani na wakwe zako kwa sababu wanaamini kwamba umemsaliti kijana wao kwa kutembea na Rayvanny na hii ni mara baada ya kuona kondomu iliyokuwa kitandani wakati mkishuti….
NANAH: Unajua hata kama ni kweli hiyo kondomu ilikuwa pale kitandani, lakini haiwahusu wao wala haimhusu mtoto wao ambaye alikuwa mchumba wangu.
IJUMAA WIKIENDA: Kwa hiyo kwa sasa upo vizuri na wakwe zako? NANAH: Mimi sina wakwe na wala sijawahi kuwa na wakwe.
IJUMAA WIKIENDA: Unaposema huna wakwe unamaanisha nini?
NANAH: Nina maisha yangu ninayoishi, hata kama niliwahi kutambulishwa, nilikuwa ninajiweka mbali sana na wao kwa sababu nilipendana na mtoto wao hivyo siwezi kujilazimisha kuipenda familia nzima au niwafosi wao familia nzima wanipende mimi, eti kwa sababu mtoto wao amenipenda.
IJUMAA WIKIENDA: Lakini ni kweli kwamba ulikuwa unatoka na Rayvanny kimapenzi?
NANAH: Siyo kweli. Mimi sijawahi kutoka kimapenzi na Rayvanny, tulifanya kazi, tukamaliza na kila mtu akashika hamsini zake.
IJUMAA WIKIENDA: Unawaambia nini watu ambao kutwa hupenda kukuhusisha kwenye ugomvi wa Rayvanny na mkewe, Fahyma kila siku?
NANAH: Hao watu wananiunganisha kwenye ugomvi wa Rayvanny na mke wake kwa sababu hawajui ukweli ulivyo, wala hawajui chanzo cha ugomvi wa wawili hao ni nini, ndiyo maana huwa ninawaacha tu waendelee kuongea kwa sababu midomo ni yao.
STORI: MEMORISE RICHARD, DAR
