RAIS John Magufuli amesema kuwa hatosita kuwawajibisha watendaji wake ambao watakuwa wazembe ama watafanya kazi kinyume na taratibu na sheria za nchi, hivyo ameagiza watumishi na watendaji wote wa serikali atakaowateua katika awamu ijayo na waliopo wachape kazi kwa manufaa ya taifa na si kwa manufaa yao binafsi.
Amesema hayo leo Novemba 13, wakati akifungua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma na kuonyesha dira ya miaka mitano ya serikali yake ambapo imejikita katika kuboresha uchumi na maisha ya wananchi wake ikiwemo kurahisisha mambo mbalimbali katika sekta ya uwekezaji na biashara sambamba na kuweka miundombinu madhubuti ya anga, majini na barabara ili kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara pamoja na huduma za kijamii.
Baadhi ya mambo muhimu aliyoyasema katika hotuba yake ni yafuatayo:
“Nitashirikiana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kulinda Amani, hatutokuwa na utani hata kidogo na mtu atakayetaka kuvuruga amani na kuingilia uhuru wetu. Namuahidi Rais Dkt. Mwinyi nitampa ushirikiano wa kutosha katika kukamilIsha aliyoyaahidi.
“Tutaendelea kuinua uchumi wa Wananchi wetu kwa kuwapa mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu, kuna mifuko mbalimbali ya kuinua uchumi ukiwemo wa Vijana na Wanawake, Waziri Mkuu kazi yako ya kwanza ikawe hii ikiwezekana baadhi ya mifuko iuanganishwe.. Wawekezaji wasisumbuliwe, Watanzania ni Matajiri ila wanaogopa kuwekeza nchini kwa kuhofia maswali mengi, tunataka Mabilionea wengi wakiwemo Wabunge, Watanzania wahamasishwe kuwekeza pesa kwenye Mabenki yetu, wakati wa kufanya mambo bila uoga ni sasa.
