×

Kaze Aanza Kazi na Programu Maalumu Yanga

 

 

KOCHA Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze, ameanza kukinoa kikosi chake jana Alhamisi baada ya mapumziko mafupi huku akiwa na programu maalumu akisubiria nyota wake waliokuwa timu za taifa.

 

Yanga imeanza mazoezi jana Alhamisi tayari kwa kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 20 baada ya kupisha timu ya taifa, Taifa Stars ambayo inacheza leo nchini Tunisia katika mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, amesema kuwa, kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo jana kocha ameandaa programu maalumu kwa wachezaji wake huku akiwa anasubiria nyota wengine.

 

“Kocha ameandaa programu maalumu kwa wachezaji wake wote waliopo hapa ili waanze nazo, wakati akisubiria wachezaji wengine warudi katika timu ya taifa ili waweze kujumuika kwa pamoja, kwa sasa anahitaji kukiunganisha kikosi chake pamoja ili kupata wachezaji watakaokuwa na ushindani mkubwa kwenye ligi.

 

“Kwa muda ambao ligi ilikuwa imesimama alikuwa akikinoa kikosi cha timu B kilichokuwa kinajiandaa na michuano ya Taifa Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni,” alisema Bumbuli.

 

Yanga ipo nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 24, nyuma ya Azam FC yenye pointi 25 ambapo imefanikiwa kushinda michezo saba kati ya 10 iliyocheza huku ikijikuta ikitoa sare michezo mitatu.

Khadija Mngwai, Dar es Salaam

Leave a Comment