×

Majaliwa Atoa Siku 4 Sakata la Bei Saruji – Video

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku nne kuanzia leo hadi kufikia Novemba 20, wakuu wa mikoa kupita kwenye viwanda na maghala ya saruji waangalie kwa nini bei ya bidhaa hiyo imepanda bila sababu ya msingi huku akiongeza kuwa katika kipindi cha uchaguzi wafanyabiashara walijisahau wakadhani serikali haiwezi kufanya chochote.

 

“Nakushukuru sana Rais kwa kunipa nafasi tena, Mheshimiwa Rais utaunda Baraza la Mawaziri muda mfupi ujao jukumu langu ni kusimamia utendaji kazi wao, nitapita kila Wizara kuwataka waweke mpango kazi wa yale yaliyoainishwa kwenye Ilani na kwenye hotuba yako. Tutaendelea kutenda yale ambayo wananchi wanayatarajia, nitasimamia malengo yaliyowekwa na ofisi yako pamoja na yaliyopo katika Ilani ya CCM ili kuwafikia Watanzania wote.

 

“Kumeibuka na upandaji wa bei ya saruji ambao hatukuutarajia bila sababu ya msingi, hatutarajii saruji kuwa na bei kubwa, inawezekana walijisahau wakadhani tupo kwenye uchaguzi kwamba hatutafanya kitu chochote.  Mheshimiwa Rais nataka kukuhakikishia kwamba nataka nianze na hilo.

 

“Wakuu wa mikoa wapo hapa Ikulu Chamwino, nawaagiza hadi tarehe 20 wawe wameenda kwenye kila kiwanda cha saruji waulize kwa nini bei imepanda hadi elfu tatu na elfu nne.  Tunahitaji maelezo kwa nini bei ya saruji imepanda, wakati serikali haijaongeza kodi,” amesema Majaliwa.

 

Leave a Comment