×

Taifa Stars Kibaruani Tena Kesho kwa Mkapa

KESHO timu ya Taifa ya Tanzani  (Taifa Stars) ina kibarua cha kusaka pointi tatu kwenye mchezo wa kufuzu Afcon 2021 dhidi ya Tunisia.

Stars ikiwa kundi J ina kibarua cha kupindua meza kibabe kwa kuwa mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0 nchini Sudan.

 

Tayari wameshaanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 4:00 usiku kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, kesho Jumanne Novemba 17, huku Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije ameweka wazi kuwa watatumia faida ya uwanja wa nyumbani kusaka matokeo.

 

“Tutakuwa nyumbani na ninaamini kwamba utakuwa ni mchezo wenye ushindani lakini tupo tayari kufanya vizuri, hivyo mashabiki watupe sapoti,” amesema.

 

Aidha, Rais wa TFF Wallace Karia, amewaomba Watanzania kuiombea Taifa Stars ili iweze kushinda kwenye mechi yake ya marudiano dhidi ya Tunisia itakayopigwa kesho Jumanne.

 

Naye Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, ametoa sababu ya mchezo kati ya Taifa Stars na Tunisia kuchezwa kesho saa 4:00 usiku akisema; “CAF walikuja na hoja ya haki ya matangazo ya televisheni na wakisema hawawezi kubadilisha na kama kuna changamoto kiusalama tuingize 25% ya mashabiki.”

 

Pia, Hersi Said, katibu wa kamati ya ushindi ya Taifa Stars amesema: “Tunajua tuna mchezo mgumu sana dhidi ya Tunisia, lakini kama kamati tumeshafanya jitihada kubwa kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri lakini hatuwezi kufanikisha bila mashabiki kuisapoti timu yetu. Mashabiki wa michezo tuache kuzungumza yale ya ugawanywaji wa klabu zetu, mashabiki wa Simba na Yanga pamoja na klabu zingine tunawaomba kuisapoti Taifa Stars, tuweke mbali mapenzi ya klabu zetu tuje tuungane kama Taifa moja.”

 

Mwamuzi Celso Armindo Alvacado, raia wa Msumbiji ndiye ‘Pilato’ atakayepuliza kipyenga kesho Jumanne, kwenye mchezo wa kufuzu AFCON kati ya Taifa Stars dhidi ya Tunisia.

 

Kwenye kundi J Tanzania ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi tatu, imeshinda mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja, ambapo inakutana na vinara wa kundi hilo ambao wana pointi tisa kibindoni. Ili kufufua matumaini ya kuweza kufuzu Afcon ni lazima ishinde kesho ili kuongeza mtaji wa pointi kibindoni.

 

Mchezo wa kesho mashabiki wataruhusiwa kuingia ila sio kwa kiwango kikubwa kwa kuwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) limetoa muongozo kwa kuruhusu asilimia 50 ya mashabiki kuingia kutokana na kuchukua tahadhari dhidi ya Corona.

Leave a Comment