RAIS wa Marekani ambaye pia alikuwa anatetea kiti chake kwa tiketi ya Chama cha Republican, Donald Trump, kwa mara ya kwanza amekiri kuwa mpinzani wake, Joe Biden ameshinda uchaguzi huo uliofanyika Novemba 3, 2020, licha ya hapo awali kuyakataa matokeo na kutangaza kwenda kuyapinga mahakamani.
Trump kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema: “Ameshinda uchaguzi kwa kuwa mchakato wa uchaguzi ulikuwa wa wizi,” lakini baada ya dakika chache alisema hamaanishi kuwa alishindwa uchaguzi huo.
Trump alirudia tena madai yake ya kuibiwa katika uchaguzi. Alifungua kesi kuhusu madai yake lakini hakutoa ushaidi wowote wa madai yake ya kuibiwa. Mashtaka yake yote yamepuuzwa.
Ijumaa iliyopita, maofisa wa uchaguzi walisema uchaguzi ulifanyika katika usalama zaidi katika historia ya Marekani na hakuna ushahidi kuwa kura zilipotea au kuibiwa au kuwa na tatizo lolote la kufanya uchaguzi kutiliwa shaka. Pamoja na ufafanuzi huo, Trump hakukubali kuwa Biden alishinda uchaguzi mpaka sasa.
Maelfu ya wafuasi wa wa Trump waliandamana Washington DC Jumamosi kupinga madai yao kufutwa. Maandamano ya amani yalikumbwa na vurugu majira ya jioni baada ya wafuasi hao kuanza kufanya fujo. Maofisa walisema watu 20 wameshtakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kushambulia watu na umiliki wa silaha.
Tukio moja la mtu kuchomwa kisu liliripotiwa, na polisi wawili kujeruhiwa. Kwa sasa kuna msukumo mkubwa kwa Trump kujiandaa kukabidhi utawala. Wakala wa huduma ya uongozi (GSA) ambao ni wakala wa serikali, wana jukumu la kuanza mchakato wa kuwatambua Biden na makamu wake Kamala Harris kuwa washindi.

