
POLISI Mkoa wa Pwani inawashikilia watu tisa wanaotuhumiwa kuchoma moto nyumba ya aliyekuwa diwani mteule wa kata ya Kikongo, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, na kusababisha vifo vya watu sita, akiwemo diwani huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, alisema mmoja wa watuhumiwa hao ni mwanamke ambapo wanatuhumiwa kuchoma moto nyumba ya diwani huyo saa 7:00 usiku wa Novemba 9, 2020.
Alifafanua kwamba katika tukio hilo watu sita wa familia moja, akiwamo diwani, Fatuma Ngozi, walifariki dunia, wawili wakipoteza maisha siku hiyo na wengine kwa nyakati tofauti wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali za Tumbi Kibaha na Muhimbili jijini Dar es Salaam.