
KOCHA mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck anatarajia kukichuja kikosi chake kabla ya msimu wa sikukuu ya kuanza kwa michuano ya kimataifa dhidi ya Plateau United ya Nigeria ambapo asiye na kiwango hatokuwa na nafasi katika kikosi hicho.
Simba inatarajia kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuvaana na Plateau United ya Nigeria ambapo mchezo wa awali unatarajia kuchezwa kati ya Novemba 27-29 huku mchezo wa marudiano ukipigwa katika Dimba la Mkapa kati ya Desemba 4-6.
Simba inashiriki michuano hiyo ya ligi ya mabingwa huku ikiwa na kumbukumbu ya kuondolewa katika hatua ya awali mwaka jana 2019 na UD Songo ya Msumbiji.
Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu wa Simba, Arnold Kashembe, amesema kuwa, kocha Sven anasubiria kikosi hicho kikamilike ili aweze kufanya maandalizi yake kuelekea katika michuano ya kimataifa na ligi kwa ujumla.
“Kocha Sven anasubiria wachezaji wote wakamilike kikosini ndipo atakapoangalia ufiti wa kila mchezaji wake kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya kimataifa kwa kuangalia wachezaji majeruhi na wale ambao hawapo fiti, lengo likiwa na kikosi kilicho imara.
“Mchakato wetu wa upatikanaji wa visa upo katika hatua za mwisho na wakati wowote tutakamilisha zoezi hilo ambalo tulilianza mapema ili kuondokana na usumbufu,” alisema Kashembe.
Khadija Mngwai, Dar es Salaam