×

Tinampay Atuma Ujumbe, Pialali Ajibu Kibabe

 

Bondia Idd Pialali (kushoto) akimjibu mpinzani wake Arnel Tinampay baada ya kupokea ujumbe wake katika mkutano wa utambulisho wa pambano la lao la kimataifa akiwa na promota Kapteni Seleman Semunyu (katikati) na mtangazaji Jimy Kabwe.

TAMBO zimezidi kupamba moto kuelekea pambano kali la kimataifa la ngumi kati ya bondia Mtanzania, Idd Pialali na Mfilipino, Arnel Tinampay, ambapo Mfilipino huyo ametamba kuwa atamchakaza mapema Pialali mbele ya Watanzania wenzake huku Pialali akijibu kwamba Mfilipino huyo ajiandae kwa kichapo kikali.

 

Pambano hilo la kimataifa litapigwa kwenye ukumbi wa Next Door Arena, Masaki Jijini Dar es Salaam Novemba 28, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, moja kwa moja kutoka Ufilipino, Tinampay anayetarajiwa kuwasili leo saa saba mchana alisema: “Nitakupiga, Pialali mbele ya Watanzania wenzako.”

 

Bondia Pialali alijibu  kwa kusema:  “Mimi siongei sana ila huyo Mfilipino inabidi ajipange kwa sababu atakutana na kichapo cha hatari.”

 

Pambano hilo limedhaminiwa na Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, DSTV, Plus TV, Precision Air, Smart Gin, Kebby’s Hotel na Uhuru FM ambapo pia siku hiyo litashuhudiwa pambano jingine la kimataifa kati ya bondia Mtanzania, Salim Mtango, kutoka Tanga ambaye atapanda ulingoni kuzichapa na Eduardo Mancito wa Ufilipino.

 

Mbali ya mapambano hayo usiku huo kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi  kati ya Adam Chiga dhidi ya Adam Kipenga, Ramadhani Shauri dhidi ya Salehe Mkalekwa, Japhet Kaseba vs Iman Mapambano, Selemani Kidunda kutoka JWTZ atazichapa na Said Mbelwa, na Ismail Caliatano pia wa JWTZ akizipiga na Mustafa Doto.  Kwa upande wa kina dada, Stumai Muki atamalizana na Lulu Kayage.

Leave a Comment