
MKURUGENZI wa Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, amesema serikali imetangaza kuwa mfanyakazi ambaye hatawasilisha namba ya mlipa kodi (TIN number) hadi Desemba 31, mwaka huu hatalipwa mshahara wa Januari
Aliyasema hayo juzi Novemba 18, wakati akizungumza na chombo kimoja cha habari ambapo amesisitiza kwamba kila mfanyakazi anayelipwa mshahara anatakiwa kuwasilisha namba yake ya mlipakodi kwa mwajiri wake.
“Kila mwajiri anatakiwa kuwasilisha namba ya mlipakodi za waajiri wake kwenye malipo. Mchakato huu utakwisha Desemba 31, baada ya hapo mfanyakazi ambaye hatawasilisha, hatapata mshahara wa Januari, hii ni kwa wafanyakazi wote Tanzania,” alisema.
Kayombo alifafanua kuwa mfanyakazi anapokatwa kodi katika mshahara wake, inatakiwa iende TRA ikionyesha kiasi kilichokatwa kwa mtumishi na namba ya mlipakodi.
“Lengo la kufanya hivi ni kwamba huu ndiyo utaratibu ambao unatumiwa duniani, tumechelewa kwa kuwa kila mlipakodi anatakiwa kulipa kwa TIN yake.
“Kilichokuwa kikileta utata kwa baadhi ya waajiri walikuwa wanasema wanalipa kodi nyingi, tukiwaomba watuletee hiyo kodi nyingi wanayolipa, wanaleta kodi ya mshahara ambayo siyo wao wanalipa bali mfanyakazi,” alisema na kuongeza kwamba mabadiliko hayo yatasaidia kuondoa utata huo na kuainisha nani analipa kodi gani na itaonekana moja kwa moja.