
MARA nyingi imetokea kwa wanamuziki wa kada mbalimbali duniani kuwika na ngoma moja tu matata mno ya kiwango cha Dunia kisha kupotea. Hili limeonekana ni tatizo kubwa. Uchunguzi wa IJUMAA SHOWBIZ umebaini si kwamba huwa hawatoi mikwaju mingine mikali, lakini tatizo linakuwa ni aina gani ya ngoma wanazotoa ambazo huwa zinashindwa kabisa kufikia ukubwa wa ngoma hiyo moja hivyo kuonekana kama hawapo tena kwenye gemu.
Hili linajitokeza kote duniani, lakini Kibongobongo listi ni ndefu mno. Anzia kwa akina Adili (Peke Yangu), Balozi (Kwenye Chati), Chelea Man (Usiniache), B-Boy (Sina Demu), JI (Kidato Kimoja), Bablee (Kizizi), Buibui (Nimekusamehe), H-Mbizzo (Mchumba) na wengine kibwena.
Hawa wote ni wanamuziki ambao uwezo wao haukutia shaka hata kidogo kwenye ngoma zao hizo. Sitaki kuamini kwamba walibahatisha kama baadhi ya mashabiki wanavyosema.
Yote hii ni matokeo ya kutengeneza ngoma kubwa ambayo baadaye hugeuka kuwa kipimo cha mafanikio makubwa, hivyo ngoma yoyote anayotoa mwanamuziki husika baada ya hapo, inakuwa kama kipimo cha mafanikio kuona kama umeweza au umepuyanga.
Inapotokea mwanamuziki akashindwa kufikia malengo ya mashabiki wake ndipo kupuuzwa huanza na kuonekana amepotea kabisa.
Haya yamewakuta wanamuziki wengi huko nyuma na sasa jinamizi linajitokeza kwa baadhi ya wanamuziki wa sasa. Miongoni mwao anatajwa Mo Music ambaye jina lake halisi ni Moshi Katemi.
Huyu ni mwanamuziki aliyejitambulisha vyema na mkwaju wake mkali wa Basi Nenda. Kwa kifupi, Basi Nenda ilikuwa ni ngoma kubwa mno, pengine tofauti na matarajio yake na sasa ameshindwa kabisa kufikia kiwango hicho.
Wengi walifananisha uimbaji wake na Marlaw huku wengine wakishindwa kumtofautisha na Becka kwenye ngoma yake ya Narudi Kazini.
Hatimaye siku zimekwenda fasta mno na mashabiki wake wakawa na shauku ya kumsikia tena Mo Music kwenye mkwaju mwingine.
Alipofurukuta, akaachia Ngoma ya Almasi, watu hawakumuelewa na hata alipotoa Ngoma ya Simama, bado waliguna na hata kwenye Nitazoea, bado walipata shida kumuelewa.
Nilichogundua ni kwamba, si kwamba Mo Music hatoi mikwaju mikali tena, hapana ila kinachomtafuna ni Basi Nenda kwani ameshindwa kabisa kutengeneza kazi itakayofika pale au kuizidi na mbaya zaidi anachoimba ni muendelezo wa Basi Nenda.
IJUMAA SHOWBIZ limefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na Mo Music ambaye anafunguka ishu ya yeye kudaiwa kwenda na Nenda Basi;
IJUMAA SHOWBIZ: Mashabiki wako wangependa kufahamu kwa sasa Mo Music una projekti gani sokoni?
MO MUSIC: Nina ngoma mpya inayokwenda kwa jina la Maumivu ambayo mpaka sasa ina wiki mbili tangu niiachie hivyo bado inaendelea kupenya mdogomdogo.
IJUMAA SHOWBIZ: Ngoma hiyo umefanya mwenyewe au umemshirikisha mtu mwingine?
MO MUSIC: Sijamshirikisha msanii yeyote, nimeamsha popo mwenyewe.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwenye ngoma hiyo hujapitia changamoto yoyote kwenye kuiandaa?
MO MUSIC: Changamoto hazikosekani, lakini mtu unatakiwa ukabidiliane nazo tu, hakuna jinsi.
IJUMAA SHOWBIZ: Ngoma ya Basi Nenda ilifanya poa nab ado inaendelea kukimbiza hadi sasa, hongera kwa hilo…
MO MUSIC: Ahsante sana, ninashukuru.
IJUMAA SHOWBIZ: Labda una lipi la kuzungumza juu ya ngoma hiyo?
MO MUSIC: Ni ngoma ambayo imeweza kunifanya nikajulikana na kuwa juu mno kwenye gemu la Bongo Fleva.
IJUMAA SHOWBIZ: Baadhi ya mashabiki wako wanadai kwamba baada ya kutoa ngoma hiyo, ngoma zote zilizofuatia zimefanya kama kukuzima kabisa, hauvumi na kwamba umeondoka na Nenda Basi, unadhani unafeli wapi?
MO MUSIC: Hakuna sehemu yoyote ninayofeli na kila ngoma ninayotoa ni inapokelewa kwa shangwe na watu ambao
kwa upande wako hili limekaaje?
MO MUSIC: Ninawaahidi mashabiki wangu kuwa mwakani mwanzoni nadhani itakuwa kwenye mwezi wa tatu, lazima nitaachia ya kwangu.
IJUMAA SHOWBIZ: Na kwenye EP yako umewashirikisha wasanii gani?
MO MUSIC: Nimewashirikisha wasanii wa kurap kutoka ndani na nje ya Bongo.
IJUMAA SHOWBIZ: Muziki wa sasa umekuwa na vita kali, kila msanii anataka kuwa juu ya mwenzake, kwa upande wako umejipanga vipi kuhakikisha unabaki kileleni?
MO MUSIC: Mimi kwa ukweli wa Mungu sishindani kabisa na mtu yeyote yule, ninashindana na kazi zangu mwenyewe kwa sababu ninafanya kile ambacho moyo wangu unaniruhusu nifanye na kinakubalika kwa mashabiki wangu.
IJUMAA SHOWBIZ: Ngoma zako fundi ni wewe mwenyewe au kuna mkono wa mtu?
MO MUSIC: Kila kitu ninafanya mwenyewe. Ni kipaji ambacho nimejaaliwa na Mwenyezi Mungu na ninamshukuru mno kwa hilo.
IJUMAA SHOWBIZ: Umefanya kolabo na baadhi ya wasanii wa Bongo, vipi kuhusiana na kolabo za nje au za kimataifa?
MO MUSIC: Ni mipango pia, ukitaka kufika mbali zaidi unatakiwa kuwa na subira, kuna kazi ambazo tayari nimeshazifanya kilichobaki na kungoja muda sahihi wa kuzitoa.
IJUMAA SHOWBIZ: Unaamini kiki kwenye muziki wako?
MO MUSIC: Hapana, mimi ninaamini kwenye kazi bora.
IJUMAA SHOWBIZ: Kwa nini huamini wakati wasanii wengi wanafanya hivyo ili kuinua muziki wao?
MO MUSIC: Sioni faida yoyote ya kufanya hivyo kwa sababu kiki siyo kitu kizuri, kinaweza kukupoteza kabisa kwenye ramani.
IJUMAA SHOWBIZ: Unapitia changamoto gani kwenye kazi yako?
MO MUSIC: Kikubwa ni kwamba sina menejimenti (wasimamizi) kwenye kazi zangu hivyo ninapitia wakati mgumu mno kwani kila kitu ninajisimamia mwenyewe.
IJUMAA SHOWBIZ: Unajivunia mafanikio gani kwenye muziki wako?
MO MUSIC: Kwa kiasi chake ninamshukuru Mungu, ninaweza kuhudumia familia yangu. Pia nimeweza kuwapa wazazi wangu biashara kubwa tu.
IJUMAA SHOWBIZ: Ukiachilia mbali kazi ya muziki, unajishughulisha na kitu gani kingine? MO MUSIC: Ninajishughulisha pia na biashara ya madini.