×

Mwenyekiti, Mtendaji wa kijiji Matatani kwa Ufisadi

WANANCHI wa vitongoji vitano vya Majengo, Nkalango, Mabambasini, Bombani na Kampuni katika Kijiji cha Ibutamisuzi kata ya Mbutu wilayani Igunga mkoani Tabora wamewatuhumu viongozi wao wa serikali ya kijiji kwa kuuza eneo la kijiji hicho lenye hekari 1,200 kwa mfugaji pamoja na kula fedha Sh milioni tano za kijiji hicho.

 

Viongozi wanaotuhumiwa kuuza eneo hilo ni pamoja na Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji hicho, Benedictor Golani Mangwiwa na Mtendaji wa Kijiji, Ludovick Ngassa.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijiji hapo baadhi ya wananchi hao, Kizanga Luhende, Mwashi Kulindwa, Hadija Jeremia na Lazaro Jackson kwa nyakati tofauti walisema viongozi wao waliuza eneo hilo kwa mfugaji mmoja bila kushirikishwa.

 

Walimtaja mfugaji huyo kuwa ni Mtakatifu Masheni Mboje mkazi wa Kijiji hicho lakini hawakuweza kutaja kiasi cha fedha alichotoa mfugaji huyo kwa viongozi hao wa kijiji.

 

Aidha, Hadija Jeremia aliongeza kuwa pamoja na viongozi hao kuuza eneo hilo, pia wamekula Sh milioni tano fedha ambazo zililipwa na mkulima waliyemtaja jina moja la Kagi aliyekodi hekari 1000 za eneo la kijiji kwa gharama ya Sh milioni l. 5 ili alime zao la pamba.

 

“Kwa kweli sisi wananchi wa Ibutamisuzi hatuko tayari kuona mali ya kijiji ikiliwa na viongozi wachache wasiowaaminifu, endapo eneo hilo na fedha hizo hazitorudishwa na viongozi hao, tutakwenda kumuona Rais Magufuli,” alisema Lazaro Jackson Jackson.

 

Hata hivyo, wananchi hao walisema fedha hizo Sh milioni tano wanazihitaji kujenga nyumba ya mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ibutamisuzi ambayo imeanguka na kusababisha mwalimu huyo kuishi mjini Igunga.

 

 

Pia wananchi hao walisema mfugaji huyo amekuwa akikodisha maeneo hayo kwa wafugaji wengine kwa ajili ya malisho kwa gharama ya Sh, 30,000 kwa heka hali ambayo imekuwa ikileta migogoro katika kijiji hicho.

 

Kwa upande wao viongozi hao wa serikali ya kijiji hicho cha Ibutamisuzi, Mtendaji Ludovick Ngassa na mwenyekiti wake Benedictor Mang’wiwa nao walijitetea baada ya kuulizwa kuhusu ya tuhuma hizo mbili za kuuza eneo la kijiji na kula Sh milioni tano.

Licha ya kukiri eneo hilo kuchukuliwa na mfugaji huyo pamoja na hizo kupotea, walidai kuwa wao hawahusiki katika tuhuma hizo.

 

 

“Sisi hatuhusiki, waliohusika na tuhuma hizo ni viongozi waliopita, kwa sababu ni kweli mfugaji huyo Mtakatifu Masheni Mboje ndiye aliyechukua eneo la Kijiji lenye hekari 1200 na kula Sh milioni tano kwa kushirikiana na uongozi uliopita,’ alisema mwenyekiti na mtendaji wake wa Kijiji.

 

Aidha, Mfugaji huyo Mtakatifu Masheni Mboje alikiri kumiliki hekari hizo 1200 pamoja na kuchukua fedha hizo Sh milioni tano.

Alisema kwa kuwa eneo hilo alipewa na uongozi wa serikali ya kijiji, mwananchi ambaye anaona hakuchukua fedha na eneo hilo kilalai aende mahakamani.

 

 

Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ya Mbutu, Lucas Bugota (CCM) alithibitisha kutambua tuhuma hizo.

Aidha, aliutupia lawama uongozi wa kijiji hicho kwa kushindwa kufuatilia suala hilo ili mfugaji uyo aweze kurudisha eneo hilo na fedha alizochukua.

Alisema yeye binafsi alifuatalia masuala hayo kwa mfugaji huyo bila mafanikio kwani mfugaji huyo amekuwa mbabe kwa wananchi hali iliyosababisha wafugaji wengine kukosa maeneo ya malisho.

 

STORI: ABDALLAH AMIRI, TABORA

Leave a Comment