
KOCHA mkuu wa timu ya Lipuli FC, Meja Abdul Mingange ameitabiria Simba SC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na ubora wa kikosi chao ambacho kinaongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye ligi.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mingange amefunguka kuwa iliuweze kuwa bingwa ni lazima timu yako iwe na uwezo wa kufunga mabao mengi, jambo ambalo Simba wanalifanya kwa kuwa timu inayoongoza kwa idadi kubwa ya mabao ambapo imefunga jumla ya mabao 29.
“Unapokwenda kucheza na timu kama Simba ni lazima uingie kwa tahadhari, Simba kwa sasa ni timu bora kwenye ligi hivyo ni lazima uingie kwa kuwaheshimu lakini ukicheza kwa kufunguka unajiweka kwenye hatari ya kufungwa mabao mengi zaidi.
“Kwa jinsi kikosi chao kilivyo ninawapa asilimia kubwa za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, kwani ili uweze kuwa bingwa ni lazima kikosi chako kiwe na uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi,” alisema Mingange.
Kikosi cha Simba kimesafiri Jumanne na sasa kipo nchini Nigeria kuvaana na Plateau United kwenye mchezo utakaopigwa wikiendi hii.
Hussein Msoleka, Dar es Salaam