
KIKAO cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kwa ajili ya kuwajadili wanachama 19 walioapishwa Novemba 24, 2020 kuwa wabunge wa viti maalum bila ridhaa ya chama hicho.

Kikao hicho kinachofanyika leo Ijumaa Novemba 27, 2020 jijini Dar es Salaam kinaongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wengine waliohudhuria ni makamu mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohammed; katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika naibu wake Zanzibar, Salum Mwalimu huku makamu mwenyekiti bara, Tundu Lissu akishiriki kwa njia ya mtandao.

Hata hivyo hadi saa 7:00 mchana walengwa wanaotakiwa kuhojiwa ambao ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza walikuwa hawajafika.