
KATIKA kuelekea maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zilizoanza Novemba 25 hadi Disemba 10, mwaka huu, jamii imetakiwa kuongeza nguvu katika mapambano ya ukatili wa kijinsia.
Hayo yanakuja ikiwa ni miaka 25 ya Beijing, China ambapo kaulimbiu ni ‘mabadiliko yanaanza na mimi’.
Akizungumza wakati wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Ofisa Program ya Harakati na Ujenzi wa Nguvu za Pamoja, Anna Sangai amesema kuwa, jamii ina wajibu wa kuhakikisha kuongeza nguvu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
“Kampeni hii imeanza Novemba 25 na itamalizika Desemba 10.
“Kwa Dunia nzima, kila asasi huwa zinafanya vitu ambavyo vitakuwa vikihamasisha kutokomeza ukatili wa kijinsia hivyo basi sisi TGNP tutafanya maadhimisho siku ya Desemba 8 na tutafanyia katika Viwanja vya (TGNP), kwa hiyo niwaomba tuungane kwa pamoja na ikiwezekana kila mmoja amuahamasishe na mwingine ili aje kuungana katika kupinga ukatili.

“Kuna lile kundi liliahidi kuimba nyimbo, tunaomba lije lioneshe nyimbo zao za kuhamasisha kupinga ukatili wa kijinsia na kutakuwa na mabango ambayo yatakuwa na uhamasishaji wa kupinga ukatili.
“Na kama mjuavyo, siku hiyo itakuwa ni siku muhimu kwa kuwa itakuwa miaka 25 ya TGNP na pia miaka hiyohiyo ya Beijing hivyo itakuwa siku ambayo tunajivunia na kuongeza nguvu ya mapambano mpaka yafike kikomo.
“Tumeona namna ambavyo uchumi unaadhirika kutokana na ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya famili kama tulivyowasikia wana jamii wenyewe walivyosema kuwa ni muda watapoteza katika kufatilia kuanzia Polisi hadi hospitali, wanapoteza kipato na mambo mengine hivyo wanajamii wameiomba Serikali kuwe na fungu ambalo litasaidia hata ikiwa mhanga ametokea, wakienda sehemu za huduma wahudumiwe kwa haraka na hata sehemu ambayo inahitajika pesa Serikali iweze kusaidia ili kutokomeza ukatili wa kijinsia,” alimaliza kusema.