
MASHABIKI wa mchezo wa soka nchini Uingereza wameruhusiwa kurejea viwanjani kushuhudia michezo mbalimbali huku wakisisitizwa kufuata utaratibu wa kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa Covid-19 ambao bado upo nchini humo.
Mchezo wa Arsenal dhidi ya Rapid Vienne wa Europa uliochezwa usiku wa jana na kumalizika kwa Arsenal kupata ushindi wa mabao 4-1 kwenye dimba la Emirates, umeingia kwenye historia ya kuwa miongoni mwa michezo ya kwanza kushuhudiwa na mashabiki baada ya vizuizi kwisha Uingereza.
Mashabiki wapatao 2,000 wameshuhudia mchezo huo huku wengi wao wakieleza kufurahishwa hatua hiyo.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema hamasa ya mashabiki imechangia kwa kiwango kikubwa vijana wake kushinda mchezo huo.
Serikali ya Uingereza, kupitia Waziri Mkuu, Boris Johnson, imetangaza kuendelea kuruhusu mashabiki kurejea kushuhudia michezo mingine kwenye Ligi Kuu (EPL) huku wakifuata tahadhari baada ya vilabu kupaza sauti kutaka mashabiki kurejea viwanjani ili waondokane na ukata.