
WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne akicheza dakika 311 bila kufunga, kocha mkuu wa kikosi hicho, Cedric Kaze amesema bado mchezaji huyo anahitaji muda ili kujenga hali ya kujiamini.
Mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso mwenye rasta, mara ya mwisho kufunga ilikuwa Oktoba 3, mwaka huu wakati Yanga ikishinda 3-0 dhidi ya Coastal Union.
Baada ya hapo, katika mechi saba zilizofuata Songne hajafunga bao ambapo ametumia dakika 311 akifanikiwa kutoa asisti mbili kwa Deus Kaseke kwenye mchezo dhidi ya Azam FC na JKT Tanzania.
Jumla Songne ametumia dakika 564 akiwa amecheza mechi 12 kati ya 13 akikosekana mechi moja dhidi ya Namungo ambapo Yanga ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1.
Kaze ameliambia Spoti Xtra kuwa, bado ana imani na uwezo wa Songne kwa kuwa anahitaji muda zaidi wa kucheza ili ajenge hali ya kujiamini. “Ni suala la muda kwake kuwa imara, kwa sasa anahitaji apewe muda na kujengwa kisaikolojia ili awe bora, ninaamini baada ya muda kila kitu kwake kitakuwa sawa,” alisema.
LUNYAMDZO MLYUKA, Dar es Salaam