×

Yanga: Tumewalipia Kisasi Simba

SI unajua Ruvu Shooting iliifunga Simba bao 1-0 Oktoba 26 kwenye Uwanja wa Uhuru! Basi juzi mashabiki wa Yanga walikuwa na jeuri kubwa walipowachapa wababe hao wa Simba bao 2-1 na wakasikika wakitamba jukwaani: “Tumewalipia kisasi.”

 

Fully Maganga aliwachapa Simba bao pekee dakika ya 36, lakini juzi vijana hao wa kocha Charles Mkwasa wenye msemaji mwenye maneno mengi, Masau Bwire, walijikuta wakikalishwa na Yanga ambayo inaonekana haikamatiki msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

 

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, bao la kwanza la Yanga lilifungwa na Mghana Michael Sarpong dakika ya 31 na sasa amefikisha mabao manne katika chati ya wafungaji, akionekana anakuja kimyakimya kileleni mwa chati hiyo.

 

Deus Kaseke angeweza kuipa Yanga bao la pili dakika ya 57 lakini kipa wa Ruvu, Abdallah Rashid alipangua penalti ya Kaseke iliyotokana na Renatus Abros kushika shuti lililopigwa na Mukoko Tonombe ndani ya eneo la hatari.

 

Dakika mbili baadaye mambo yakawa mabaya kwa Yanga baada ya Bakari Mwamnyeto ambaye alikuwa chini ya kiwango juzi, kumzawadia pasi David Richard akiwa ndani ya boksi na bila hiyana, akauweka mpira kimiani.

 

Baada ya bao hilo, Yanga hawakukata tamaa, waliendelea kulisakama lango la Ruvu na dakika ya 63, Sarpong alipiga shuti akiwa ndani ya boksi lililokwenda nje kidogo ya lango.

 

Dakika tatu baadaye, kashkash katika lango la Ruvu, ilisababisha Cassian Ponera ajifunge akiwa anakabana na Sarpong baada ya pasi ya Tuisila Kisinda.

 

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Yanga imezidi kujikita kileleni ikiwa na pointi 34, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 26, inayotarajiwa kucheza dhidi ya Gwambina leo Jumatatu ugenini jijini Mwanza.

 

Matokeo hayo yanamaanisha pia kuwa Yanga imewaacha mahasimu wao, Simba ambao ni mabingwa watetezi kwa tofauti ya pointi 11.

 

Simba ina viporo vingi ikiwa imecheza mechi 11, ikiwa na pointi 23, Yanga imecheza mechi 14, ikiwa na pointi 34. Kama Simba wakishinda viporo vyao vyote vitatu ambavyo inaanza kuvila keshokutwa Jumatano dhidi ya Polisi TZ kwenye Uwanja wa Mkapa, watakuwa na pointi 32 na watabakiza pointi mbili tu kuifukia Yanga kileleni.

 

Yanga imeweka rekodi ya kufungwa mabao matano tu katika mechi 14 ilizocheza. Hii ndiyo timu iliyofungwa mabao machache zaidi hadi sasa kwenye ligi msimu huu, sawa na Simba ambayo nayo imefungwa matano katika mechi 11 ilizocheza.

 

Yanga walioanza: Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong, Deus Kaseke na Yacouba Songne.

 

Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, Kabasele Hamad, Cassian Ponera, Renatus Ambros, Juma Nyosso, Zuber Dabi, Mohammed Issa, Shaban Msala, Fully Maganga, David Richard, Abdulrahman Mussa.

 

Matokeo mengine:- Mtibwa Sugar 1-0 Mwadui FC, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Ihefu FC 1-1 JKT Tanzania, Uwanja wa Sokoine.

SAID ALLY, Dar es Salaam

Leave a Comment