
BENCHI la Ufundi la Simba limedhamiria kuwapa mapumziko mafupi nyota waliokuwa wakitumikia timu za taifa ili kuwaweka sawa kabla ya kukumbana na wapinzani wao FC Platinum ya Zimbabwe.
Simba inashuka dimbani leo Jumatano kuvaana na Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo pia wanakabiliwa na mchezo wa hatua ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Platinum utakaochezwa kati ya Desemba 22-23 na kurudiana Januari 5-6, baada ya kukamilisha viporo vya ligi.

Nyota wa Simba ambao walikuwa wakizitumikia timu zao za taifa ni pamoja na kiungo Clatous Chama, Luis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco, Jonas Mkude na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambao kwa mujibu wa Kocha Sven anahitaji kuwapa muda wa kupumzika ili kuendelea kuimarika zaidi kikosini.
Akizungumza na Championi Jumatano,Meneja wa Simba, Abass Ally, amesema kuwa, wakati wakiwa wanaendelea na maandalizi ya mechi ya Ligi ya Mabingwa, Kocha Sven yupo katika mchakato wa kuwapa mapumziko baadhi ya nyota ambao wametumika sana huku wakiendelea na mechi za ligi kutokana na kutumika sana kwa lengo la kuwaimarisha zaidi.“
Kabla ya kukutana na Platinum tuna mechi tatu za ligi dhidi ya Polisi Tanzania tutakaocheza nao Jumatano, Mbeya City na Namungo kisha tunaelekeza nguvu zetu katika mchezo dhidi ya Platinum, kikosi kipo kambini na Ijumaa kinatarajia kuondoka kuelekea Mbeya.
“Baadhi ya wachezaji wametumika sana wamecheza ‘back to back’ hivyo kocha ameona ni vyema awape muda wa kupumzika japo hata siku mbili kisha waendelee na kucheza kama hawa waliokuwa timu ya taifa ya Tanzania, wametoka kucheza na Tunisia kisha wamerudiana hapa nyumbani.

“Baada ya kumaliza majukumu ya kuitumikia timu ya taifa walisafiri na timu kwenda Arusha kucheza mechi za ligi kisha tumesafiri nao kwenda Nigeria kucheza mechi dhidi ya Plateau na sasa mechi za ligi.
“Hivyo wanahitaji kupata muda wa kupumzika hata siku mbili ili waweze kuwa fiti na kuendelea na kazi ya kuipigania timu yao kuhakikisha wanarudi katika viwango vyao kwa kuwa miili imechoka,” alisema Abass.Hata hivyo inaelezwa kuwa kocha huyo amesema atakuwa akiwapumzisha kwa kupishana na siyo wote.
Stori: Khadija Mngwai,Dar es Salaam