
ARUSHA: HATUA ya kikongwe mwenye umri wa miaka 101, Nderekwa Ndesaulo Ayo kuamua kujichimbia kaburi lake akisubiri mauti yamfike, limewaacha vinywa wazi wakazi wa Kijiji cha Nambala, Kata ya Kikwe wilayani Arumeru, mkoani Arusha yalipo makazi yake.
Kikongwe huyo mwenye watoto 10 wajukuu na vitukuu ambao idadi yao haikufahamika, amedai kuchukua uamuzi huo kwa sababu ana hofu ya kuzikwa mbali na malkia wake (mkewe) aliyefariki miaka mitano iliyopita na kuzikwa kwenye eneo la nyumba yao.
Amesema, iwapo watoto wake na ndugu wengine watabadilisha uamuzi wake na kumzika sehemu nyingine ameandika wosia wa laana kwao. Mke wa kikongwe huyo aitwaye Lipina Lyatuu alifariki mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 91.
Akizungumza na mwandishi wetu hivi karibuni mzee huyo alisema, kwa kuwa mwanadamu lazima afe na kwamba naye anataraji kufa siku si nyingi na kuingia kwenye nyumba yake hiyo ya milele aliyojijengea ameona ajiandalie kabisa mahali pa kuzikwa.
“Mpaka sasa nimetumia zaidi ya shilingi milioni moja kuchimba kaburi na kujengea, bado kulifunika tu, baada ya hapo nabaki nikisubiri siku zangu za mwisho wa kuishi duniani zitimie.
“Nimeogopa kuzikwa porini baada ya kusikia sheria ya mipango miji inayotaka marehemu wazikwe makaburi ya umma mimi sitaki kuzikwa mbali na nyumbani kwangu nataka nizikwe pembeni ya mke wangu,” alisema.
Aliongeza kuwa, kabla ya kufikia uamuzi wa kufanya jambo hilo aliwashirikisha ndugu na jamaa ambapo walimkatalia lakini hakusitisha zoezi hilo.
“Nataka siku ya kifo changu watu wasilie, bali washereheke kwa kula na kunywa kwa sababu Mwenyezi Mungu amenipa uhai kwa miaka mingi,” alisema.
Wakizungumzia hatua ya baba yao kujijengea kaburi wakati akiwa hai baadhi ya watoto wake akiwemo Riphaty Ayo, aliyezaliwa mwaka 1948, alisema jambo hilo liliwashtua kiasi cha kumkataza mzee wao asifanye hivyo lakini ilishindikana kutokana na msimamo wake mkali.
“Kwa kweli mzee alisisitiza azikwe jirani na mke wake na asipelekwe kokote hata kama sheria ya mipango miji inakataa na amenipa barua ya kumjulisha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ila bado sijaipeleka,” alisema Ayo.
Naye Eliyakisinde Ayo, mtoto wa tano na Yose Ayo mtoto wa sita wa kikongwe huyo walisema hatua ya baba yao kujichimbia kaburi imewasononesha kwani kila wanapolitazama hilo kaburi hutokwa na machozi kutokana na kuamini kuwa baba yao ni kama amekufa na kwamba anasubiri kuzikwa kwenye kaburi hilo.
“Tulipambana kumsihi baba asijichimbie kaburi kwa sababu ni sawa na kujichulia kifo, mzee alitukatalia kabisa imebidi tuizoee hali hii,” alisema Yose.
Joseph Ngilisho, Uwazi