×

Wasanii Watano Bongo Kuwania MTV Awards

WASANII  watano wa Tanzania akiwemo Diamond Platnumz wametajwa kuwania tuzo za MTV mama 2021,  zitakazofanyika jijini Kampala Uganda mapema mwakani.

 

Wasanii wengine wa Tanzania waliotajwa kushiriki tuzo hizo ni Harmonize, katika kipengele cha msanii bora wa kiume, Zuchu (msanii anayechipukia), Rostam (kundi bora la muziki) huku Diamond yeye akiingia kwenye vipengele viwili (msanii bora wa mwaka na shoo kali kipindi cha corona).

 

Tuzo za MTV Mama zinazotarajiwa kufanyika nchini Uganda mapema 2021, zitahusisha zaidi ya wasanii 30 kutoka mataifa 15 ya Afrika, huku kwa mara nyingine wasanii kutoka Nigeria wakitawala kwa kutajwa mara 14 kwenye vipengele vya tuzo hizo.

 

Katika tuzo hizo za kimataifa zinazofanyika kila mwaka kipo kipengele kipya kwa ajili ya kumtunuku msanii aliyepiga shoo kali kipindi ambacho nchi nyingi duniani zilikumbwa na ugonjwa wa corona na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama.

 

Katika kipengele hicho, Diamond ameingia kutokana na kutumbuiza na ubunifu alioufanya kwenye tamasha la kuchangia familia zilizokumbwa na janga la Covid-19, tamasha lilikofanyika Mei, 2020 la Africa Day Benefit Concert.

 

Majina ya washiriki wa tuzo hizo zenye vipengele 10 yalitangazwa usiku wa kuamkia leo Desemba 10, 2020, ikiwa ni pamoja na kufungua rasmi pazia kwa mashabiki kuanza kuwapigia kura wasanii wanaowapenda, ambapo kura hizo zinapigwa kupitia tovuti ya mtvmama.com.

 

Tuzo za MTV Mama zilianzishwa mwaka 2008 maalumu kwa ajili ya wanamuziki wa Afrika na kila mwaka taifa moja kutoka barani humo hupewa kibali cha kuwa mwenyeji. Kwa Afrika Mashariki ni Kenya na Uganda waliowahi kupata kibali hicho.

Leave a Comment