×

Mke Alia Mumewe Kufanyiwa Kitu Mbaya na Mwenyekiti

LOGATI Jonathan ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Maretoni, Kata ya King’ori – Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, ameiomba Serikali kumchukulia hatua kali Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maretoni, Juma Bulele ambaye anatuhumiwa kumjeruhi vibaya mumewe aliyefahamika kwa jina la Edward Msemakweli (26).

 

Logati ambaye ni mke wa Msemakweli alidai kuwa siku ya tukio mumewe aliondoka nyumbani usiku kwenda kununua vocha lakini cha ajabu alivamiwa na mwenyekiti huyo na kushambuliwa na jiwe hadi kupoteza fahamu.

 

“Hili tukio limenisikitisha sana kwani mume wangu ndio namtegemea kwa kila kitu hivi sasa hatuna chakula watoto wanalala na njaa hatuelewi tufanye nini tunaomba serikali ichukue hatua kali kwa huyu mhusika” alisema.

 

MAJERUHI AZUNGUMZA

Akizungumza kwa shida Msemakweli alisema tukio hilo limetokea katika kitongoji hicho Novemba 25 mwaka huu muda wa saa tano usiku.

 

Alisema baada ya mwenyekiti huyo kumkuta akiongea na simu na kuchukua jiwe na kuanza kumshambulia sehemu za siri ambazo zimesagika. Msemakweli ambaye ni fundi ujenzi, amelazwa katika hospitali ya Mkoa Mount Meru baada ya kufanyiwa operesheni ya utumbo na sehemu za siri zililokuwa zimesagika kutokana na kupondwa na jiwe na mwenyekiti huyo.

 

Alisema siku ya tukio alitoka nyumbani kwake majira ya usiku na kwenda kununua vocha ili aweze kuwasiliana na fundi mwenzake kwa ajili ya kumpatia vifaa vya ujenzi ili kesho yake aweze kuamkia kibaruani.

 

Alifafanua kwamba akiwa anaongea na simu kando kidogo na eneo la duka, ghafla alitokea mwenyekiti huyo na kumuuliza kwanini unaongea na simu muda huu usiku ukiwa peke yako.

 

Alisema mwenyekiti huyo ambaye alionekana kuwa katika hali ya ulevi aliokota jiwe na kuanza kumshambulia kwa kumpiga tumboni mara kadhaa na kuanguka chini ambapo alianza kumpiga na jiwe hilo sehemu za siri jambo lililofanya apoteze fahamu.

 

“Baada ya kunipiga nilisikia maumivu makali sana na kuanguka chini nilishindwa kujitambua na baadaye nilizinduka na kujikuta nipo katika hospitali nimelazwa sikujua kilichoendelea,”alisema Msemakweli.

 

BABA NAYE ANENA

Aidha, baba mkwe wa majeruhi, Jonathan Palangyo anayemuuguza majeruhi huyo alidai kwamba, maelezo ya daktari yanaonyesha aliumia sehemu ya tumbo.

 

“Kwa mujibu wa daktari ni kwamba utumbo mpana umekatika, sehemu za siri zimesagika hivyo uwezekano wa kuzalisha utakuwa mdogo… kwa kweli hili jambo limetuhuzunisha sana maana hatuelewi sababu hasa za kumtendea ukatili huo ni nini,” alisema.

 

Hata hivyo, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Salumu Hamduni alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akidai kwamba mtuhumiwa anashikiliwa na uchunguzi unafanyika ili kuhakikisha anafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.

Stori: Joseph Ngilisho, Arusha

Leave a Comment