×

Mmoja Mbaroni Mauaji ya Mwanafunzi

JESHI la polisi mkoani Mwanza linamshikilia Hamis Omary mwenye umri (19) mkazi wa Nyasaka kwa tuhuma za mauaji. Mtuhumiwa alinadaiwa kutekeleza unyama huo katika kata ya Kawekamo wilaya ya Ilemela kwa kumuua mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Katunguru aliyejulikana kwa jina la Vincent Renatus umri (17).

 

Kamanda wa jeshi la mkoa wa Mwanza, Muliro Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mwanafunzi huyo alikutwa ameuawa katika chumba chake alichokuwa akiishi na mwili wake ukiwa na majeraha pamoja na kuporwa vitu mbalimbali vya ndani ikiwemo radio na televisheni.

 

Muliro ameeleza kuwa jeshi la polisi baada ya kupata taarifa walifanya msako mkali ulioongozwa na taarifa za kiintelijensia na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa. Alieleza kuwa baada ya kufanya mahojiano na mtuhumiwa alikiri kuhusika na mauaji ya mwanafunzi huyo.

 

Muliro alieleza kuwa mtuhumiwa aliwaonesha askari vitu walivyopora kwenye chumba cha marehemu na kwenda kuviuza kwa Erasto Jackson mkazi wa Kitangiri amabaye na yeye amekamatwa kwa mahojiano kwa uhalifu sugu wa kupokea mali za wizi.

 

“Jeshi la polisi hatushindwi na jambo lolote… mtuhumiwa amefanyiwa mahojiano na kukutwa na tuhuma hizo, kwanza jambo ambalo amelifanya ni la kikatili sana” alisema muliro. Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ili kuwaweza kufanikisha kuwakamata wahalifu na kuacha tabia ya kukaa kimya.

STORI; CONSOLATA EVARIST, Amani

Leave a Comment