
KUNDI la muziki la Scopion Kings kwa kushirikiana na mkali wa Afro Pop, Tresor kutoka Afrika Kusini, wameachia singo mpya iitwayo ‘Funu’ ambayo inaendelea kufanya vizuri kwenye mitandao mbalimbali duniani.
Katika kolabo hiyo, Scopion Kings linaloundwa na Kabza De Small na Maphorisa wakipiga mahadhi ya Kwaito wakiwa na Tresor ambaye ni bingwa wa Afro Pop, wameachia singo ‘Funu’ kama kibisha-hodi tu, kwani albamu nzima inayokwenda kwa jina la ‘Rumble In the Jungle’ yenye jumla ya nyimbo 14 itaachiwa mapema mwezi Februari, mwakani.
“Hiki ni kipindi cha majira ya joto barani Afrika, ni wakati wa kusherehekea Scorpion Kings ambao kwa pamoja wameungana na muasisi wa Afro Pop, Tresor ili kuachia albamu kali ‘Rumble In the Jungle.
“Ni albamu yenye nyimbo kali 14, ambayo inapatikana kwa oda kwa kuagiza mapema kwenye Apple Music, lakini itatoka rasmi Februari 2021,” ilisema taarifa kutoka kwa watayarishaji.
“Ndani ya Rumble In the Jungle, utasikia sauti tamu katika ushirikiano wa watatu hao – Tresor, Maphorisa na Kabza De Small ambazo zina mchanganyiko wa ladha za muziki wa Amapiano na Afro House. Ni kazi nzuri na tamu,” iliongeza taarifa hiyo.
Funu ni wimbo ulioimbwa kwa ustadi mkubwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ambao mirindimo yake itakupa uthibitisho kuwa watatu hao ni moto wa kuotea mbali.
Na Joseph Shaluwa