
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Katarina Zebedayo (38), mkazi wa Kijiji cha Kabanga Kata ya Ilangu, Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, amefariki dunia baada ya kula nyama ya nguruwe pori na wengine nane kulazwa katika kituo cha afya Mishamo kwa matibabu.
Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Benjamin Kuzaga alisema kuwa, tukio hilo lilijiri Disemba 11, mwaka huu, muda wa saa tisa Alasiri katika Kijiji cha Kabage Kata ya Ilangu.
Alisema kuwa, katika tukio hilo, wananchi wa kijiji hicho waliona mnyama adhaniwaye kuwa ni nguruwe pori akiwa amekufa porini, jirani na mashamba yao, ndipo walipomchuna ngozi na kugawana nyama na kuondoka nayo majumbani kwa ajili ya kitoweo.
Kamanda Kuzaga aliwataja waathirika wengine katika tukio hilo kuwa ni Leonard Kabula (17,) Sifa Kabula (04), Levis Kabula (03), Boniphace Kabula (01), Seth Eliya (30), Lidness Mayokolo (09), Noadia Balasiano (36) na Sostenes Phillipo (01); wote wakazi wa Kijiji cha Kabanga.
Wananchi hao wanadaiwa kuwa baada ya kutumia kitoweo hicho na kupata madhara, walianza kutumia dawa za kienyeji mpaka mmoja wao kuzidiwa na kufariki dunia ndipo mwenyekiti wa kijiji hicho, Theodoli Philipo (30), akabaini na kufanya jitihada ya kuwafikisha waathirika wengine kwenye Kituo cha Afya cha Mishamo.
Kamanda Kuzaga alisema baada ya mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi huku sampuli zikiwa zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi kubaini sumu iliyosababisha kifo pamoja na madhara kwa watu hao.
Aidha, aliongeza kuwa, waathirika wote wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye Kituo cha Afya cha Mishamo na hali zao zinaendelea vizuri.
Pia aliwataka wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi kutojihusisha na uwindaji haramu na kuacha tabia ya kula vitoweo ambavyo vinakuwa vimekufa kwenye mazingira ambayo si salama ili kuweza kujiepusha na madhara yanayoweza kuepukika.
STORI: WALTER MGULUCHUMA, KATAVI