×

Somalia Yasitisha Uhusiano na Kenya, Yatimua Wanadiplomasia

 

SOMALIA imetangaza kusitisha uhusiano wake na Kenya ikidai kwamba serikali ya Kenya inaingilia kati masuala yake ya ndani.

 

Nchi hiyo jirani wa Kenya, imetangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walio Nairobi kurudi Mogadishu ndani ya siku saba kuanzia leo (Jumanne) Desemba 15 2020.

 

Waziri wa habari wa Somalia Osman Abukar Dubbe, amesema katika hotuba iliyorusha moja kwa moja na televisheni ya serikali ya Somalia Jumatatu jioni kwamba hatua hiyo imechukuliwa kujibu uchokozi wa kisiasa wa kila mara unaofanywa na serikali ya Kenya kinyume na uhuru wa Somalia.

 

 

Wakati huohuo, serikali ya Kenya haijajibu  hatua  ya Somalia kumwondoa balozi wake nchini Kenya Novemba 29 na kuamuru balozi wa Kenya kuondoka Mogadishu kwa madai kwamba (Kenya) kuwa inaingilia masuala yake ya ndani na siasa za nchi hiyo.

 

Somalia ilidai Kenya ilikuwa “inamshinkiza kisiasa” kiongozi wa eneo la Somali, Ahmed Mohamed Islam maarufu kama Ahmed Madobe wa Jubaland, ili kutimiza malengo yake ya kisiasa na kiuchumi ndani ya Somalia.

 

Somalia inadai kwamba kutokana na ushawishi wa Kenya, Ahmed Madobe alilegeza msimamo wake kuhusu mkataba wa Septemba 17, mwaka huu, kati ya serikali kuu na viongozi wa maeneo.

 

Mkataba huo ulikuwa wa kutoa fursa ya kufanyika uchaguzi usio wa moja kwa moja nchini Somalia lakini kiongozi wa eneo Jubaland sasa anataka serikali ya Somali kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Gedo ili utawala wake uandae uchaguzi ambapo hatua hiyo inapingwa na serikali kuu.

Leave a Comment