×

Yanga Wafuata Kiungo Sauzi

INAELEZWA uongozi wa Yanga upo katika mchakato wa kunasa saini kiungo mshambuliaji wa Kaizer Chiefs ya Afrika katika usajili wa dirisha dogo unaotarajiwa kufunguliwa wiki ijayo.

 

Tayari mazungumzo na kiungo huyo anayefichwa na maofisa wa timu hiyo kwa lengo kuwahofia wapinzani wao Simba yamekamilika kwa asilimia 70 huku wakipanga kuachana na kipa wao Mkenya Faroukh Shikhalo.

 

Yanga ambayo inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 34 imekuwa katika mkakati wa maboresho wa kikosi cha timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo ikiwemo kumshusha kiungo ambaye anatajwa kuwa bora katika pasi za mwisho.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Ijumaa limezipata kutoka maofisa wa ndani wa timu hiyo alisema kuwa tayari Yanga imekaribia kukamilisha usajili wa kiungo huyo lakini bado wamekuwa wakifanya siri kwa kuficha jina lake kwa kuhofia kuhujumiwa.

 

“Ni kweli kuna mchezaji kutoka Kaizer Chiefs, anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, kocha ameshapewa faili lake na wakati wowote huenda uongozi ukamaliza naye kwa sababu wanakata kusitisha mkataba na Shikhalo ambao upo mwishoni ili aweze kuingia huyo mchezaji.

 

“Unajua wenyewe wameshajua kwamba kuna watu wamekuwa wakivujisha taarifa za ndani na wamekuwa wakifanya uchunguzi mkubwa ili waweze kuwabaini lakini suala la huyo kiungo lipo tayari isipokuwa bado amekuwa akifichwa na uongozi juu ya majina yake,” alisema mtoa taarifa.

 

Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Cedric Kaze alivyotafutwa alisema kuwa kwa sasa bado anaendelea na wachezaji wake waliopo katika kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri katika mechi zilizobaki hivyo ni ngumu kuanza kuzungumzia mambo ya usajili.

Ibrahim Mussa na Wilbert Molandi, Dar

Leave a Comment