
BEKI wa Simba ambaye anamudu pia kucheza kama kiungo mkabaji, Erasto Nyoni, amesema kuwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waendelee kutoa sapoti yao kwani mchezo wao wa kwanza ugenini dhidi ya Platinum FC wanakwenda kushinda.
Nyoni alisema kufanya vizuri kwenye michezo ya ligi kuu wakiwafunga Mbeya City na KMC kumewapa nguvu zaidi kuelekea katika mchezo huo na ari na morali ya wachezaji ipo juu na hata upungufu kidogo ulioonekana benchi la ufundi wataufanyia kazi ili kwenda kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Akizungumza na Championi Ijumaa Nyoni alisema wana kila sababu ya kwenda kushind mchezo huo kwa sababu ari, morali na nguvu yao ni kubwa sana na kufanya vizuri katika michezo ya ligi kumewaongezea kujiamini na wao kama wachezaji wanasubiri kupewa mbinu kutoka kwenye benchi la ufundi, ingawa kila kitu kipo sawa hadi sasa.“
Napenda kuwaambia mashabiki na Wanasimba wote kuwa wasiingie unyonge labda kwa sababu tunakwenda kucheza ugenini, wajue tu kwamba tunakwenda kushinda huo mchezo, ari na morali yetu sisi kama wachezaji ipo juu, tunasubiri benchi la ufundi wafanye kazi yao tu,” alisema Nyoni.

Simba wametinga katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwaondosha Plateau United ya Nigeria kwa jumla ya bao 1-0 na Desemba 23 watacheza na Platinum FC nchini Zimbabwe kabla ya kurudiana Januari 6, 2021.
Stori: Issa Liponda