×

Lwandamina Aomba Muda Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Mzambia, George Lwandamina, yupo katika mchakato wa kumchunguza nyota mmojammoja katika kikosi hicho ili kupembua pumba na mchele ili kujua nyota gani anastahili kuongezwa katika kikosi hicho ambapo ameomba muda katika kukamilisha zoezi hilo.

 

Lwandamina ametua Azam FC hivi karibuni kuchukua nafasi ya Mromania, Aristica Cioaba aliyetimuliwa kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo inayosuasua hadi sasa kwenye ligi.

 

Azam FC ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 28 ikiwa imecheza mechi 15 na kupoteza michezo mitatu, sare nne huku ikishinda michezo 8, lakini lengo lake ni kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema kuwa, kocha Lwandamina ameomba apewe muda kwa ajili ya usajili katika kikosi hicho ili aweze kuwachunguza nyota wake wote kwa kujua nani anafaa na nani hafai.“

 

Usajili wetu utategemea mapendekezo ya mwalimu Lwandamina, kwa sasa anahangaika kuwajua wachezaji wake ili kujua wachezaji gani aweze kuwasajili katika dirisha dogo, kwa sasa yeye ni mgeni, hamjui mchezaji hata mmoja, hivyo anahitaji muda kuweza kuwaangalia wachezaji wake.“

 

Anaweza kusema asajili mchezaji fulani kumbe yule anayemhitaji yupo katika kikosi chake, hivyo anakuwa hajafanya kitu, hivyo anaangalia mchezaji mmojammoja kiwango chake kisha atatupatia ripoti ambayo ndio tutaanza kuifanyia kazi kabla ya dirisha kufungwa, ana muda wa kutosha kuweza kuangalia wachezaji wake,” alisema Zakazi.

Leave a Comment