×

Vita Ya Harmo, Wasafi Yafika Pabaya

DAR: Upepo haujatulia! Wakati Watanzania wakiendelea kufurahia muziki mzuri kutoka kwao, nyuma ya pazia kunafukuta bifu zito kati staa wa Bongo Fleva, Rajabu Abdul ‘Harmonize’ na wafuasi wa lebo yake ya zamani, Wasafi Classic Baby (WCB), Gazeti la IJUMAA linakupakulia habari kamili.

 

Historia inaonesha, Harmonize au Harmo tangu ajiengue Wasafi, amekuwa kwenye msigano wa matukio mbalimbali ambayo kimsingi yanaonesha dhahiri kuwa, hayupo sawa na ama wafuasi wa lebo yake hiyo ya zamani au timu nzima ya Wasafi.

 

MONDI ANASEMA WAKO SAFI…

Kuhusu timu ya Wasafi, bosi wao, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema hana kinyongo na kijana wake huyo ambaye amemtambulisha kwenye gemu na anamtakia kila la heri kwenye mafanikio yake.

 

TUANGALIE TUKIO BICHI

Tukio ambalo ni la hivi karibuni linalotafsiri kwamba hali si hali, linadaiwa kutokea ndani ya Maduka ya Mlimani City jijini Dar ambapo watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Wasafi (Team Wasafi), wanadaiwa kumvaa Harmo na kuanza kumzomea.

 

Kwenye klipu ambayo Gazeti la IJUMAA linayo, anaonekana Harmo akiwa anatembea peke yake kwenye korido za maduka hayo na sauti za watu hao zikisikika kumzomea huku wakimuambia kwamba amefulia kwani kwa sasa anatembea bila mabodigadi.

 

MANENO MAKALI

Watu hao walimshambulia Harmo kwa maneno makali na kumwambia kwamba ameishiwa hivyo asitegemee hata kidogo kama anaweza kupambana na Mondi kwani ni kama ardhi na mbingu na ameshapoteza dira ya kimuziki.

Watu hao walionekana kumzonga Harmo kiasi cha kumfanya akose amani licha ya kwamba naye alikuwa bize na shughuli zake kwenye maduka hayo.

 

MATUKIO MENGINE

Matukio mengine ambayo yanatajwa kuwagusa moja kwa moja Harmon a Wasafi ni pamoja na lile la mmoja wa mameneja wa Mondi, Sallam SK ‘Mendez’ kuelezwa kuwa ndiye aliyemchoma kwa aliyekuwa mlezi wa WCB, Paul Makonda kwa kumueleza kuwa Harmo anatumia ‘sigara kubwa.’

 

Malumbano kwenye suala hilo yaliendelea hata pale Harmo alipojitoa Wasafi ambapo ilifika mahali, meneja huyo alishindwa kupokea salamu ya Harmo alipokuwa kwenye msiba wa mke wa Hamisi Taletale ‘Babu Tale’ ambaye alikuwa miongoni mwa mameneja wa Mondi.

 

HARMO APIGA KIJEMBE

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmo pia aliwahi kutupa kijembe kwa kuweka ‘klip’ iliyoonesha jamaa mmoja mfupi ambaye alitupa jiwe gizani kwa kusema anafanana na bosi wake wa zamani hivyo watu kutafsiri kuwa alimlenga Sallam.

 

Kama hiyo haitoshi, juzikati ilivuja ‘klipu’ ambayo ilimuonesha Harmo akiwa na mwanaye na kumwambia asilie, asiogope kwani baba yake ndiye msanii namba moja Bongo.

 

Akaenda mbele zaidi kwa kumwambia asiogope chochote na hata maneno kutoka kwa Baba Levo (mtangazaji wa Wasafi) kwani walikuwepo akina Dudu Baya (Godfrey Tumaini) na wameshindwa vita.

Baadaye Baba Levo aliibuka na kumvaa vikali Harmo na kumuonya kwamba asihangaike kupambana na Mondi kwani hamfikii hata kidogo.

 

HUJUMA ZATAJWA

Kwenye mwendelezo wa matukio ya utofauti wao, Harmo amekuwa akitajwa kuhujumiwa na wafuasi wa Wasafi ambao wamekuwa wakimfanyia hujuma ya kumshitaki kwenye Mtandao wa YouTube na nyimbo za Harmo zikiathirika kwa kufungiwa.

 

Hata hivyo, Harmo amekuwa akipambania na matokeo yake zimekuwa zikirudishwa na kuendelea na safari. Lakini hata hivyo, hujuma hizo zimekuwa zikikosa mashiko au ushahidi wa moja kwa moja kama kweli wanaofanya hivyo ni wafuasi wa WCB au wametumwa na viongozi wa kruu hiyo.

 

MENEJA WA HARMO ANASEMAJE?

Alipoulizwa kuhusu tukio la hivi karibuni la msanii wake kuzomewa kwenye maduka ya Mlimani City, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ anasema yeye kwa upande wake haoni kama ni tatizo na hawezi kulihusisha tukio hilo na jambo lolote.

 

“Ni matukio tu kama matukio mengine, inategemea wewe unalichukulia kwa upande gani. Mbona hukuzungumzia yale ya kushangiliwa? Yapo mengi ya kushangiliwa hivyo sioni kama ni tatizo,” anasema Mjerumani.

 

TUJIKUMBUSHE

Harmo alijitoa Wasafi mwaka jana na kwenda kuanzisha lebo yake maarufu kwa jina la Konde Gang Music Worldwide. Baada ya kujitoa, uongozi wa WCB ulimwekea ngumu kutumia nyimbo alizozalisha akiwa chini ya lebo hiyo hadi pale alipolipa shilingi milioni 500 kama ada ya kuvunja mkataba na kuanzia hapo akawa huru.

Stori: Mwandishi wetu

Leave a Comment