
MADIWANI wanawake kutoka Halmashauri 24 nchini, wameupongeza Mtandao wa Jinsia wa TGNP kwa kuwaandalia warsha ya siku nne iliyowapa mafunzo ya kuwawezesha kutimiza vyema majukumu yao ya uongozi.

Warsha hiyo imefanyika kwenye ofisi za TGNP zilizopo Mabibo Jijini Dar, ambapo wawezeshaji wenye uzoefu na masuala ya uongozi ndiyo waliokuwa wakiwapa mafunzo hayo.
Lengo la warsha hiyo ni kuwawezesha wanawake nchini kuwa viongozi bora na kufikia asilimia hamsini kwa hamsini za uongozi na wanaume.

Baada ya kumalizika kwa warsha hiyo madiwani walianza kutoa shukrani zao wa TGNP kuwaandalia warsha hiyo ambayo wamejifunza mengi ambayo walikuwa hawayajui.

“Hii mimi mara yangu ya kwanza kuwa diwani na nilikuwa sijui hata nianzie wapi katika kutimiza majukumu yangu lakini leo nashukuru TGNP kupitia warsha hii nimejifunza mambo mengi sana ambayo yatanisaidia kwenda kuboresha utendaji kwenye kata yangu” alisema Diwani wa Kata ya Sumbawanga Mjini, Leticia Kipeta.

Diwani wa Kata ya Lagana Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Samila Wilson amesema kwake msimu wa 2020-2025 ni msimu wake wa tatu na alikuwa hajawahi kupata semina kama hiyo lakini sasa hivi ameishukuru sana TGNP kwa warsha hiyo ambayo imemuwezesha kwa kiasi kikubwa sana kwenda kutimiza majukumu yake.

Doris Paulo, Diwani wa Kata ya Visiga, Pwani amesema huu ndiyo msimu wake wa kwanza kushika nafasi hiyo, hivyo warsha hiyo imemsaidia sana kujua mambo mbalimbali ikiwemo kuyajua majukumu yake.

Paskarina Ndunguru, Diwani wa Kata ya Madibila Wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya alisema;
“Semina hii imenipa mwangaza mkubwa sana katika kwenda kutimiza majukumu yangu na nawaomba TGNP waandae semina kama hizi mara kwa mara ili kuendelea kukuzana ufahamu”, alimaliza kusema Paskarina.

Karibu madiwani wote baada ya kumalizika warsha hiyo walisikika kuipongeza TGNP kwa kuwaandalia warsha hiyo iliyowapa mwangaza mkubwa katika kwenda kutekeleza majukumu yao.