×

Dimpoz: Nipo Tayari Kufanya Kolabo

BILA shaka hakuna anayeweza kubisha kuwa supastaa wa Bongo Fleva, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ ni mmoja wa wasanii wazuri ndani ya anga la muziki huu mtamu.

 

Licha ya kupitia changamoto nyingi za maradhi yaliyoathiri koo lake na hata wengine kudhani maradhi hayo yangekatisha safari yake ya kusimama jukwaani na kuimba, sasa hali imekuwa tofauti kwani ameweza kuamka tena na kuachia ngoma kadhaa kali ikiwemo Ni Wewe inayoendelea kutoboa mitaa siku hadi siku.

 

Dimpoz ambaye hivi sasa ni mmoja wa wasanii ambao watakuwa chini ya lebo kubwa ya muziki duniani- Sony, amewatoa hofu mashabiki wake kuwa hawezi kupotea hata siku moja kama watu wengi wanavyoichukulia lebo hiyo. Mbali na hilo, Dimpoz amezungumzia uwezekano way eye kufanya tena kazi kwa mara nyingine na mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Kwenye exclusive interview na OVER ZE WEEKEND, Dimpoz amefunguka mengi;

OVER ZE WEEKEND: Mambo vipi Dimpoz?

Dimpoz: Poa, habari za majukumu?

OVER ZE WEEKEND: Salama kabisa… naona sasa hali inaendelea vizuri.

 

DIMPOZ: Kabisa kwa kweli, Mwenyezi Mungu ananisaidia sana kama unavyoona niko bomba kabisa.

OVER ZE WEEKEND: Umekaa muda kidogo bila kuachia ngoma, kuna kitu kipya kinakuja?

 

DIMPOZ: Lazima ukiona kimya kingi ujue kabisa kuna kitu kinakuja, kwa sababu kutoa ngoma kila wakati ni mtihani mkubwa, inabidi ukae na kuona ni kipi unaweza kutoa na kikawa kizuri kwa mashabiki wako. Hata sasa nimeachia kitu kinaitwa Dede na kinafanya poa sana.

 

OVER ZE WEEKEND: Hilo dude umelirekodi ukiwa ndani ya Lebo ya Sony?

DIMPOZ: Ndiyo, ni kazi nzuri sana… sijisifii, lakini ni mzuri.

OVER ZE WEEKEND: Wewe ndiye ulikuwa msanii wa kwanza kufanya kazi na Vanessa Mdee, kwa pamoja mliachia ile Ngoma ya Me and You, ilimtambulisha vyema sana, vipi ulivyosikia ameamua kuacha kuimba ulichukuliaje uamuzi wake?

 

DIMPOZ: Kwa kweli kwangu niliumia kwa sababu najua uwezo wa Vanessa, lakini huwezi kumlaumu mtu kwa sababu ukweli ni kwamba mpaka anaamua hivyo ujue kuna kitu ameona au amekitafakari na kuona hawezi kuendelea, ila kwangu siku zote ataendelea kuwa msanii bora.

 

OVER ZE WEEKEND: Umekuwa ni mmoja wa wasanii waliochaguliwa kuwa ndani ya Lebo ya Sony, lakini wadau wa muziki wanasema msanii akiingia kule anashuka kimuziki, hili unalizungumziaje?

 

DIMPOZ: Watu waache uoga jamani, hakuna kitu kama hicho. Nimesikia sana kuhusu hilo, lakini halina ukweli wowote. Watu wanavyofikiria siyo sahihi kabisa…kwa upande wangu ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifanikisha kuingia Sony.

 

OVER ZE WEEKEND: Kwa hiyo utakuwa unafanya kazi chini ya Seven kwa hapa Tanzania?

DIMPOZ: Ndiyo, ni mtu wangu wa karibu na tunaelewana sana, ninaamini kabisa kazi itaenda vizuri sana.

OVER ZE WEEKEND: Ukiachilia mbali kazi ya muziki unayofanya, kuna kitu kingine unachofanya maana siku hizi tunasikia mambo yako ni safi sana?

 

DIMPOZ: Mimi niko pale GSM kwenye mambo ya masoko, ndiyo maana Mungu anazidi kututendea mambo mazuri kabisa.

OVER ZE WEEKEND: Wasanii wengi sana wamekuwa wakinadi uhusiano wao wa kimapenzi mitandaoni, lakini kwa upande wako, sijaona ukifanya jambo kama hilo, je, unaogopa kuibiwa au?

 

DIMPOZ: Siyo jambo jema, kwanza kuweka maisha yako halisi kwenye mitandao ya kijamii kuna mambo mengi sana yanaweza kukutokea.

OVER ZE WEEKEND: Wengine wanafanya mara mojamoja, kwako sijui ni kwa nini imekuwa ni vigumu kiasi hicho?

DIMPOZ: Kwa upande wangu hapana… nitamuonesha mke wangu ambaye nimefunga naye ndoa.

 

OVER ZE WEEKEND: Umekuwa ni mmoja wa majaji wa Bongo Star Search mwaka huu, kazi hiyo kwako ina changamoto gani?

DIMPOZ: Changomoto ni kubwa kwa sababu kumjaji mtu yupi anafaa na yupi hafai, ugumu unakuja pale wote wana vigezo, basi unakuwa kwenye wakati mgumu sana, lakini mwisho wa siku unakubaliana na hali halisi.

 

OVER ZE WEEKEND: Ila nasikia Madam Rita, amekulipa mkwanja mrefu mpaka umekubali kuwa jaji, ni kweli?

DIMPOZ: Ndiyo amenilipa pesa nzuri sana, lakini hata kama asingenilipa yule ni mdau mkubwa sana wa muziki wetu ambaye anainua vipaji vya vijana ambao walikuwa huko mitaani, walikuwa hata hawajui kabisa watatokea wapi, hivyo hata kama angenifuata bure mimi ningefanya.

 

OVER ZE WEEKEND: Mara nyingi Ngoma ya Nani Kama Mama’ uliofanya na Christian Bella umekuwa ukiimbwa, popote ulipo unatoa machozi, ni kwa nini?

DIMPOZ: Ni kwa sababu ninapata hisia za kweli kabisa kwenye moyo wangu, labda pia kuna mengine yananigusa kabisa mimi moja kwa moja.

 

OVER ZE WEEKEND: Ilikuwa ikifahamika kuwa wewe na baba yako, Faraji Nyembo, hamkuwa sawa, vipi sasa hivi mmeweka kando tofauti zenu?

DIMPOZ: Baba ni baba siku zote, sina tatizo naye, ninamuombea kwa Mungu siku zote ampe maisha marefu aje kuona mpaka wajukuu wake.

 

OVER ZE WEEKEND: Sasa hivi ukitakiwa kufanya kazi moja kali na Diamond kama mlivyofanya zamani, uko tayari kufanya naye kolabo?

DIMPOZ: Kabisa, nipo tayari, kwa nini nisifanye naye? Sisi ni wasanii ambao ni kioo cha jamii. Siwezi kuacha kwa sababu hatuna tatizo kubwa kama watu wanavyofikiria.

 

OVER ZE WEEKEND: Mimi naomba nikushukuru sana kwa ushirikiano wako…

DIMPOZ: Asante sana, nifikishie salamu zangu Global. Pia ninampongeza sana Mkurugenzi Shigongo kwa kuteuliwa kuwa mbunge. Hakika anastahili.

 

Makala: IMELDA MTEMA

Leave a Comment