
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa Desemba 23, 2020 alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji tuzo kwa washindi mashindano ya TEHAMA yaliyoandaliwa na kampuni ya HUAWEI ambapo Tanzania imeshika nafasi ya pili kidunia na ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahala.
Katika hotuba yake Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi kutumia vizuri Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hasa katika shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali ili kusaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kufikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye maeneo mengi zaidi kwa lengo la kuongeza matumizi ya mawasiliano ya kasi (broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia 80 ifikapo mwaka 2025.
Waziri Mkuu amesema ili kufikia malengo hayo, Serikali itatoa kipaumbele kwenye masuala ya tafiti na ubunifu sanjari na kutambua na kusajili wataalamu wote wa TEHAMA nchini.

Vilevile, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo HUAWEI katika kuhakikisha inaanzisha vituo vya umahiri vya sayansi na teknolojia kwenye taasisi za elimu ya juu nchini kwa kuzingatia maeneo ya kimkakati katika kujenga uchumi imara na endlevu sambamba na kudhibiti athari hasi zinazoweza kutokea kutokana na matumizi ya TEHAMA.”
Waziri Mkuu pia amezitaka kampuni za ndani zinajishughulisha na masuala ya TEHAMA ziige mfano wa kampuni ya HUAWEI kwa kuwekeza zaidi kwa kundi la vijana kwa nia ya kuibua na kuendelea vipaji.