×

Mwandishi Aliyeripoti ‘Ukweli’ wa Corona Afungwa Jela Miaka 4

 

 

MWANDISHI wa habari wa China aliyekamatwa kwa ‘kuripoti ukweli’ kuhusu janga la ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona katika Jimbo la  Wuhan, China,  ametupwa jela miaka minne.

 

 

Zhang Zhan (37), ambaye ni mwanamke,  ametiwa hatiani kwa ‘uchokozi na uchochezi’ kutokana na alivyoikosoa serikali jinsi ilivyolishughulikia janga hilo lilivyoibuka.

 

Zhang, mwandishi wa kwanza raia aliyefunguliwa mashtaka, alikuwa miongoni mwa watu wachache ambao waliishuhudia hali halisi ilivyokuwa katika hospitali zilizokuwa zimejaa wagonjwa na mitaa ambayo ilikuwa haina watu, ambapo alielezea hali mbaya zaidi ya ugonjwa huo ulivyokuwa kuliko ulivyoelezewa na serikali.

 

Hata hivyo, mwanasheria wake, RenQuanniu, amesema watakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya Pudong, Shanghai.

 

Kabla ya mashtaka hayo, mwanasheria huyo alisema  aliamini kwamba mteja wake, Zhang, alikuwa anasakamwa hivyo kutokana na kutumia uhuru wake wa kujieleza.

Wakati mashtaka hayo yakiendelea, mamlaka yalikuwa yametoa onyo dhidi ya kauli zozote hususan kutoka kwa madaktari.

 

Vilevile, vyombo vya habari vya serikali vimesifia udhibiti wa virusi vya ugonjwa huo uliofanywa na uongozi wa Rais Xi Jinping.

 

Jumuia moja yenye kutetea haki za binadamu ya jijini New York, Marekani, ilisema kwamba Zhang alikuwa anaadhibiwa ‘kwa kufanya kile ambacho dunia ilitakiwa kukieleza kuhusu virusi vya corona kutoka Wuhan’.

 

Mji wa Wuhan wenye wakazi wapatao milioni 11uliingia katika nadhari ya kimataifa mwaka jana wakati virusi vya corona vilipoibuka huko na kusambaa duniani na kusababisha vifo vya watu  wasiopungua milioni 1.7duniani hadi sasa.

 

 

Huko Shanghai, polisi waliimarisha ulinzi katika mahakama hiyo ambapo mashtaka dhidi ya Zhang yalifunguliwa miezi saba baada ya kukamatwa kwake.  Pia waandishi wa habari wa nchi za nje walizuiwa kuingia mahakamani.

 

Video za Zhang, mwanasheria mstaafu, ziliwekwa katika mtandao wa  YouTube zikionyesha mahojiano yake na maoni na watu mbalimbali kwenye vituo vya treni na mahospitalini.

Alikamatwa mwezi Mei mwaka huu na mwezi Juni alianza mgomo wa kutokula, hati za mahakama zimefichua, ikiwa ni pamoja na mateso aliyofanyiwa na polisi ambapo hadi kufikia Desemba alikuwa amekumbwa na maumivu ya kichwa, tumbo, kizunguzungu, maradhi ya koo na kushuka kwa shinikizo la damu.

 

Zhang amekana madai ya serikali kwamba alikuwa ameandika na kukusanya habari za uwongo, na akasisitiza kwamba ripoti zake zote zilitokana na mahojiano aliyofanya moja kwa moja na watu mbalimbali huko Wuhan.

 

 

Leave a Comment