
WADAU wa michezo wanaojulikana kama Watawa Sports kwa kushirikiana na Chama cha Ngumi Wilaya ya Nyamagana (NDBA), wameandaa tamasha la ngumi za wazi kesho Ijumaa, siku ya mwaka mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari, mratibu wa tamasha hilo, Geofrey Katanga, amesema lengo la tamasha hilo ni kuhamasisha vijana kupenda mchezo wa ngumi kwa ajili ya kujiingizia kipato na ajira.

Pambano hilo litakuwa na buti tano ambapo wapambanaji kutoka katika wilaya ya Nyamagana na Ilemela watapambana na washindi wataondoka na kitita cha shilingi laki moja.

Aidha, mwalimu Omary Mussa kutoka Mabatini amesema maandalizi ya vijana wake yamekamilika na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vitasa kutoka kwa wapambanaji mahiri.

Mshiriki mmoja wa tamasha hilo, Yussup Jani, alijigamba kwa kusema atamtoa kwa ‘knockout’ mpinzani wake, Kennedy Mwangoto,hivyo amemtaka aje akiwa amejipanga.

Aidha, waandaaji wa tamasha hilo wamewaomba wakazi wa Jiji la Mwanza kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Shule ya Msingi Mirongo kushuhudia masubwi kwani mbali na ngumi kutakuwepo na burudani mbalimbali na hakutakuwa na kiingilio, na milango itafunguliwa kuanzia saa 3 asubuhi na mapambano yataanza saa 6 mchana.

Na Leah Marco, Mwanza