×

Aika Asimulia Msoto wa Kulala Chumba Kimoja!

 

AIKA Mariale na Emmanuel Mkono ‘Nahreel’ ni moja kati ya kapo bora za mastaa hapa Bongo. Wamedumu pamoja bila kutetereka kwa zaidi ya miaka kumi ambapo wamejaliwa watoto wawili; Jamaika na Gold.

 

Mastaa hawa wanaounda kundi la Navykenzo, wametamba zaidi na ngoma ya Kamatia Chini, ingawa watu kwa sasa wanawaona wapo kimya lakini ukweli ni kwamba ‘wanakamata mwizi kimyakimya’ kwa sababu wanapiga mkwanja mrefu kupitia bidhaa za watoto ambazo wamefungua kampuni yao wenyewe inayoitwa Gold.

 

Mikito Nusunusu ilipata wasaa mzuri wa kufanya mahojiano na Aika ambaye alisisitiza kuwa uhusiano wao una muunganiko kutoka kwa Mungu hivyo hata kama kuachana ni lazima Mungu apende na si binadamu huku wakiwa hawana habari na kifunga ndoa kwa sasa.

 

Mikito: Habari za siku Aika?

Mikito: Sal ama kabisa.

Mikito: Aika naona kwa upande wenu wewe na Nahreel mmegoma ndoa?

 

Aika: Nilishawahi kusema kabisa kuwa ndoa ni mimi na Nahreel yaani tunaweza kuamka hapa tukaamua kwenda kanisani hata usiku tukafunga tu na kurejea nyumbani maana maisha niliyokaa na Nahreel ni zaidi ya ndoa kabisa.

Mikito: Kwenye mitandao ya kijamii kila kukicha wanawaposti kama ‘kapo’ iliyogoma kuachana kabisa kama ilivyo kwa mastaa wengine…

 

Aika: Kuachana kwetu ni Mungu maana yeye ndio alituunganisha labda apange kututenganisha lakini sio maneno ya watu kabisa, watazidi kutuona kila siku tupo tu.

Mikito: Ila mmekuwa kimya kidogo na ukizingatia wakati huu ni mgumu kwa kila mmoja inakuwaje hii?

 

Aika: Maisha siku zote huwezi kutegemea kitu kimoja ndio maana ukilala ukiamka unapigana maisha yaendaje hivyo basi tukaamua tuanzishe Gold Product, maana ukweli wazo la biashara ya vitu vya watoto niliipata baada tu ya kujifungua Gold.

Mikito: Nini kilikusababisha upate hilo wazo?

 

Aika: Unajua wakati nimejifungua mama yangu aliniletea pempasi nyingi sana na ni nzuri hapohapo na mimi nikapata wazo kwa nini nisifanye hiyo kitu.

Mikito: Na ulivyoanza kufanya uliona inakusaidia kwa kukuongezea kipato?

 

Aika: Sana tu kwa kweli sijui nisemaje maisha yamezidi kuwa tofauti kabisa maana huwezi kukosa chochote sasa muhimu cha kuendelea kwenye maisha, namshukuru Mungu sana, bidhaa zote muhimu za watoto zipo kwetu na zinapendwa na tupo nchini nzima.

Mikito: Kulikuwa na tetesi kuwa uhusiano wenu uliingia doa hiyo vipi?

 

Aika: Unajua watu wengi wanapenda sana mitandao na wanapenda kuamini sana wanachokiona kwenye mitandao bila hata kujua ukweli wa maisha ya mtu mwenyewe.

Ni hivi, mimi na Nahreel hakuna wa kumuacha mwenzake kwa namna yoyote ile maana hapa tunasubiri kuongeza watoto wengine, najua watu wanatamani sana kuona hatuko pamoja lakini ndio ishakuwa na siku zinazonga mbele kila kukicha.

 

Mikito: Lazima kutakuwa na siri kubwa nyuma ya pazia ya kudumu kwa muda mrefu kwenye mahusiano yenu ni nini maana mastaa wengi wameshindwa?

 

Aika: Ukweli ni kwamba kama kuna mapenzi ya dhati kati yenu mambo madogomadogo mtayaacha yapite.

Mikito: Watu wengi wanajua mmetoka familia yenye maisha mazuri lakini mlivyoanza mwanzo historia yenu ilikuwa ni maisha ya kawaida sana.

 

Aika: Ni kweli lakini tulipambana wenyewe kwa sababu wazazi wetu walikuwa hawapendi tufanye muziki na walitupeleka shule nje ya nchi lakini muziki ulitukolea zaidi hivyo ilibidi kupambana sana ikiwa ni pamoja ya kulala chini kwa muda mrefu sana mimi na Nahreel na kushinda njaa kuanzia asubuhi mpaka jioni.

 

Tuna Mangi wetu alikuwa akitusaidia sana hatuwezi kumsahau kabisa kwenye maisha yetu hivyo tumepita msoto mkali sana lakini imetusaidia sana na tunaweza kujitegemea kwa kiasi kikubwa sana.

Mikito: Wengi wanajua pia nyumba ambayo mnaishi kwa sasa ni kwa msaada mkubwa wa wazazi wenu ni kweli?

 

Aika: Hapana kabisa, wanaotufahamu tulikuwa tukiishije wanajua kabisa maana mpaka leo chumba tulichoanzia maisha kipo, ni pembeni tu na nyumba yetu hii maana asubuhi sebule na studio, jioni chumba cha kulala hivyo watu wajue jinsi gani ya kuvumilia kwenye maisha yao ya kila siku.

 

Mikito: Unaonekana mara nyingi hujichaganyi na mastaa wengine kama ilivyo kwa wengine, hii ni kwa nini?

Aika: Sasa huwezi kujichanganya tu, lakini panapo ulazima wa kufanya hivyo unafanya na kama hamna ni vyema kutulia ili kuepuka mambo mengine.

 

Mikito: Una wivu na Nahreel?

Aika: (kicheko) kwa nini? Sana tu, tena mtu asijaribu kabisa.

Mikito: Haya asante sana kwa ushirikiano wako.

Aika: Asante sana.

STORI: IMELDA MTEMA

 

Leave a Comment