
TAFAKARI haya, baada ya miaka 24 ya ndoa, unagundua kuwa watoto watatu kati ya wanne ambao umekuwa ukiwalea pamoja na mke wako si wako halisi.
Si kwamba visa hivi hutokea kwenye filamu pekee kwani jamaa mmoja ambaye alikumbana na hali hii alithibitisha kuwa mambo haya ni ya kweli.
Kupitia mtandao wa Twitter, mkazi mmoja wa jiji la Nairobi nchini Kenya, Julius Mmasi almaarufu Khasakhala aliwaacha wanamtandao vinywa wazi baada ya kufichua kuwa rafiki wake wa karibu alilazimika kuvunja ndoa yake ya miaka 24 na mke wake baada ya matokeo ya vinasaba (DNA) kubainisha kuwa ni baba halisi wa mtoto mmoja pekee kati ya wanne ambao aliwalea pamoja na mke wake.
Jambo la kuhuzunisha zaidi ni kuwa mke wake alikiri kuwa bosi wake ndiye baba ya watoto watatu wa kwanza.
“Mwanamume huyo aliamua kufanyia watoto wake wanne uchunguzi wa DNA baada ya kuanza kumshuku mke wake.
“Kwa uchungu mkubwa, aligundua kuwa mabinti wake watatu ni watoto wa bosi wa mke wake huku kitinda mimba ambaye ni wa kiume ndiye mtoto wake pekee halisi katika ndoa hiyo.
“Watoto watatu wa kwanza wa kike, wawili walifuzu mwingine yuko kidato cha nne. Mke wake alikiri kuwa watoto watatu wa kwanza ni wa bosi wake.
“Utamshauri mtu kama huyu vipi kuhusu haya? “Ndoa ya miaka 24 imevunjika ghafla, maana kuwa wanaume wengi wakiamua kuchukua hatua hii ndoa nyingi zitavunjika,” alisema Khasakhala.
Kulikuwa na maoni mbalimbali katika mtandao huo wa Twitter baada ya Khasakhala kusimulia maswahibu ya rafiki yake.
Aidha, utafiti wa awali uliofanywa na mtandao wa Tuko nchini Kenya ulifichua kuwa asilimia 80 ya Wakenya wanaamini kuwa vipimo vya DNA vinatakiwa kuwa vya bure.
Stori: Mwandishi Wetu na Mtandao