
Wakati tumeuanza Mwaka wa 2021 leo, kuna mambo ya kuyatazama kwa kina kwenye gemu la Bongo Fleva.
Kubali au ukatae, ukweli ni kwamba Bongo Fleva ya sasa huwezi kuilinganisha na miaka ile kwani inafika mbali kwenye sayari hii ya Dunia.
Wasanii wamejua kuwapa mashabiki wao kitu roho inataka.
Baadhi ya wasanii wa Bongo Fleva wameendelea kuonesha ubunifu wa hali ya juu na kufanya kazi nzuri ambazo zitaishi miaka mingi, zikisikilizwa na kutazamwa na vizazi vijavyo kadiri Dunia itakavyodumu kwani kwa sasa Dunia imezeeka mno; ina umri wa zaidi ya miaka bilioni 4.5.
Kwa mwaka 2020, wapo wasanii ambao wamejua kutoa kazi ambazo zimebamba na zinaendelea kubamba.
Wasanii kama Diamond Platnumz, King Kiba, Harmonize, Jux, Marioo, Rayvanny, Mbosso, Nandy, Maua Sama, Darassa na wengine wengi walifanya poa mno.
Lakini sasa kuna jamaa wa kizazi kingine kipya wanakuja kwa kasi kwa lengo la kufanya mapinduzi ya Bongo Fleva na wanatabiriwa kuwa watasumbua kinoma kwa mwaka 2021.
Wakati leo tukiuanza mwaka huu wa 2021, IJUMAA SHOWBIZ inakuletea listi ya wasanii kumi (Top 10) ambao wanapaswa kutazamwa zaidi kwa mwaka huu wa 2021 kwani wanakuja juu kwa spidi ya roketi ya kwenda Sayari ya Mars;
ZUCHU
Second lady wa lebo kubwa ya muziki barani Afrika ya Wasafi Classic Baby (WCB), Zuhura Othman ‘Zuchu’ ni miongoni mwa wasanii wanaotajwa kwenye listi hii kuwa kwa mara nyingine atakiwasha kinoma.
Zuchu anazidi kufanya poa kila kukicha akifukizia cheo cha Umalikia kutokana na mambo anayoyafanya.
Mbali na kufanya ‘wandaz’, lakini pia ana nyota kali mno. Tangu atambulishwe kwenye gemu Aprili 8, mwaka jana, ameweka rekodi za kila aina.
Ni miezi nane tu tangu atambulishwe kwenye gemu, lakini habari zake zimepenya hadi nje ya Bongo ambako si rahisi kwa msanii mdogo kufika kwa haraka kiasi hicho.
Zuchu ameweza kuweka rekodi kwenye muziki wake kiasi cha kutrendi na mastaa wakubwa barani Afrika kama Diamond, Wizkid, Burna Boy, Davido na wengine.
MABANTU
Mabantu ni kundi la vijana wawili ambao wanakuja kwa kasi kama moto wa nyika.
Hawa ni mtoto wa baba mkubwa na baba mdogo, Twarha Emmanuel Kanengo na Muharami Hamisi Kajonje. Kundi la Mabantu linatabiriwa kuwa mwaka huu litakiwasha mno. Wapo baadhi wanaolifananisha kundi hili na lile la akina Peter na Paul Okoye la P-Square kabla ya halijasambaratika.
Jamaa wana kiu ya kutoboa kimataifa.
Wiki iliyopita walibonga na Gazeti la IJUMAA na kufunguka namna ambavyo wamehaso hadi hapo walipofikia.
Mwaka 2020 ndipo walipoanza kuwaka kwani waliwika na mikwaju mikali ambayo imewatambulisha vyema ndani ya Bongo na sasa ni zamu ya kutoboa kimataifa.
IBRAH
Ni dogo matata chini ya lebo kubwa inayomilikiwa na Rajabu Abdul ‘Harmonize’ ya Konde Gang Music Worldwide.
Ibraah anakuja vizuri kwenye gemu pamoja na kwamba hana papara nyingi, lakini muziki wake unapenya mdogomdogo kwenye ngoma za masikio ya wengi na muda si mrefu atajikusanyia kijiji cha mashabiki.
Tangu asajiliwe Konde Gang amekuwa akisifika kwa kufanya muziki mzuri na unaokubalika kiasi cha kutwaa tuzo na ngoma zake kutrendi kwenye mitandao ya kusikiliza, kutazama na kupakua muziki.
YOUNG LUNYA
Rapa huyu alianza kuonekana akiwa na Kundi la OMG chini ya Lebo ya Switcher Records ya mtu mzima, Quick Rocka. Alisikika na ngoma kama Umbeya ambayo alifanya na Barakah The Prince. Baadaye alisimama mwenyewe na kuanza kutoa kazi zake kama msanii wa kujitegemea.
Kisha alionekana kwenye kolabo za wasanii wakubwa kama Joh Makini kwenye Ngoma ya Mchele kisha Bedroom Remix ya Harmonize.
Pia amesikika kwenye mikwaju kama Tikisa akiwa na Country Boy, Moto na nyingine kibao. Young Lunya anatajwa kuwa atakuwa moto wa kuotea mbali mwaka huu chini ya Harmonize.
HANSTONE
Huyu ni yule dogo wa kwenye Ngoma ya Iokote aliyoshirikishwa na Maua Sama. Wakati mkwaju huo unatoka, siyo kwenye mitandao, vibanda vya simu, redio, TV, miito ya simu, Bajaj, teksi na hata bodaboda, masikio na macho ya mashabiki yalikuwa kwa Maua na Hanstone.
Huyu dogo ni mtoto wa kaka wa marehemu Banza Stone, Hassan Masanja.
Ukimsikiliza ni kama amepita mulemule kwa Diamond kuanzia staili hadi melodi.
Kwa taarifa za chinichini, kuna kila dalili akasajiliwa pale WCB chini ya Diamond. Kama ni kweli, basi ni mwaka wa Hanstone.
MC BALAA
Kwa moto anaokuja nao huyu dogo kwenye anga la Singeli, Dullah Makabila, Sholo Mwamba, Meja Kunta, Mzee wa Bwax na wengine, wanatakiwa kukaa mguu-pande. Bila hivyo, ufalme wa Singeli unakwenda kubebwa na MC Balaa.
Tayari kitaa kimemuelewa MC Balaa kutoka kwenye Singeli-Bakora na sasa anafanya Singeli-Biashara. Dogo anatabiriwa kwamba atafanya maajabu mwaka huu.
TOMMY FLOVOUR
Tommy Flavour ni nyota mpya kutoka Lebo ya Kings Music inayomilikiwa na Mfalme wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.
Ni mmoja wa wasanii wanaopaswa kutazamwa zaidi mwaka huu.
Tommy anafanya mambo makubwa kwenye muziki na ameonekana kukubalika kwa kuwa yupo kwenye mikono ya kipaji kikubwa cha King Kiba.
OFFICIAL NAI
Anaitwa Hunai Ramadhani ila kwa wafuatiliaji wa mambo yake wanamjua kwa jina la Official Nai au Mnyama Mkali.
Ni miongoni mwa ma-video vixen wakali Bongo wanaotikisa vilivyo ndani na nje ya Bongo kutokana na mambo wanayoyafanya kwenye tasnia ya burudani.
Kwa sasa Nai ametumbukia kwenye Bongo Fleva na anashika maiki ile mbaya. Tayari anasumbua na ngoma yake ya Siyo Saizi Yako.
Nai anatajwa kwenye listi ya wasanii wanaoibuka ambao watatisha mno kwa mwaka huu kama tu atakuwa ‘serious’.
MONI CENTROZONE
Jina lake halisi ni Awadh Chami. Mchanganyiko wa melodi kwenye ngoma zake unanivuta kumpachika katika gurudumu hili.
Rapa huyu amekuwa akifanya ngoma kali na akishirikiana na wasanii wakubwa kwenye gemu.
Ngoma kama Lamoto imekuwa ikitikisa mno kwenye midia na mitandaoni. Ngoma zake nyingine ni Chuchu Dede na Godoro. Uwezo wake umempa tiketi ya kushiriki kwenye ngoma ya Harmonize ya Bedroom Remix.
MIMAH
Kwa Mimah, taarifa zimfikie Mama wa Majanga, Snura Mushi kwamba asipokaa sawa, basi ataomba poo.
Mimah anatajwa kuwa mmoja wa wadada wanaokiamsha ile mbaya kwenye Uwanda wa Singeli.
Mimah anakuja kwa kasi kwenye gemu na anatajwa kwamba atafanya mapinduzi ya Singeli kwa wanawake.
MAKALA: KHADIJA BAKARI