
MBUNGE wa Buchosa, Mhe. Eric Shigongo amekutana na Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), Eng. Abdu Diganga, ambapo wamefanya mazungumzo na kutembelea eneo ambalo linatarajiwa kujengwa bandari ya kivuko kipya kitakachokuwa kikifanya safari zake kati ya Nyakaliro na Kisiwa cha Kome ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi za mbunge huyo alizozitoa katika kipindi cha kampeni.

Eng. Diganga amesema kutokana na umuhimu uliopo katika kivuko hicho, atahakikisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatekelezwa na watu wanapata huduma nzuri ya usafiri ili kuimarisha na kuweka miundombinu salama na kurahisisha shughuli za usafirishaji za wananchi hasa mazao na samaki ili kujenga uchumi na kukuza vipato vyao haraka.

Aidha, Eng. Diganga amesema tayari fedha zipo na kazi inatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia Januari hii huku akiwataka viongozi wa Serikali ya Kijiji kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kupokea mradi huo bila kuwa na malalamiko yoyote kwani barabara itakapoaanza kujengwa kuna baadhi ya mazao yataondolewa na wale ambao nyumba zao zipo karibu na barabara zitabomolewa kwani barabara hiyo ilikuwepo tangu miaka ya nyuma.

Kwa Upande wake Mhe. Shigongo amemshukuru Eng. Diganga na kumwahidi kutoa ushirikiano wa dhati ili mradi huo mkubwa uweze kukamilika kwa wakati na kutoa huduma nzuri kwa wakazi wa Kome, Nyakarilo na Buchosa nzima kwa jumla.

Na IDD MUMBA, aliyeko Buchosa